Umoja wa Ulaya (EU) na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi Duniani (UNHCR) wamesaini makubaliano mapya ya ushirikiano ili kuendeleza juhudi za kulinda na kuwapatia misaada ya kibinadamu wakimbizi na waomba hifadhi kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) wanaoishi katika Kambi ya Nyarugusu, pamoja na wale wapya wanaopokelewa katika Kituo cha mpito mkoani Kigoma, Tanzania.
Kupitia mchango wa
TZS bilioni 9.2 (sawa na EUR milioni 3), Umoja wa Ulaya unaunga mkono jitihada
za UNHCR za kutoa msaada wa haraka wa kuokoa maisha na huduma muhimu kwa
mahitaji ya ulinzi katika sekta za mbalimbali ikiwemo afya, maji na usafi wa
mazingira (WASH), makazi na elimu, zikiwemo huduma maalum kwa watu wenye
mahitaji ya kipekee waliokimbia machafuko kutoka DRC.
“Kuongezeka kwa
migogoro duniani kumesababisha idadi kubwa ya wakimbizi wanaohitaji msaada wa
haraka. Ndiyo maana leo ninajivunia kutangaza usainishwaji wa mkataba wa TZS
bilioni 9.2 (EUR milioni 3) na UNHCR hapa Tanzania. Makubaliano haya muhimu
yatanufaisha moja kwa moja wakimbizi walioko nchini, kwa kuhakikisha ulinzi
wao, kuwasaidia kuishi maisha ya heshima, na kuwawezesha kupata njia za
kujikimu. Kama Umoja wa Ulaya, tunaendelea kushikilia misingi ya ubinadamu na
mshikamano wa kimataifa. Ni lazima tuendelee kushirikiana kukabiliana na
changamoto hizi za kimataifa na kulinda haki na utu wa kila mtu anayetafuta
hifadhi,” amesema Balozi Christine Grau, Balozi wa Umoja wa Ulaya nchini
Tanzania na Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Mwaka 2025, UNHCR kwa
kushirikiana na wadau wa kitaifa na wa kimataifa, inaendelea kuiunga mkono
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kupokea waomba hifadhi wapya
wanaowasili mkoani Kigoma Kutoka DRC. Kuanzia Januari hadi Juni mwaka huu,
zaidi ya waomba hifadhi 3,000 wamepokelewa Kigoma. Wakati huo huo, UNHCR na
wadau wanaendelea kutoa huduma kwa wakimbizi wa Kongo wapatao 85,105 walioko katika
Kambi ya wakimbizi ya Nyarugusu. Wakimbizi hawa hupokea msaada wa haraka
ikiwemo malazi salama, chakula, huduma za afya, maji safi, miundombinu ya usafi
wa mazingira, pamoja na huduma nyingine muhimu.
Kutokana na hali ya
taharuki inayowalazimu wakimbizi kukimbia makazi yao — mara nyingi hufanikiwa kuondoka na nguo
walizovaa tu na mali chache wanazoweza kubeba — upatikanaji wa huduma za afya,
malazi, maji safi, usafi na mazingira salama ni muhimu sana. Huduma hizi
hupunguza vifo na magonjwa, lakini pia hulinda utu, usalama, na ustawi wa jumla
wa wakimbizi na waomba hifadhi.
“Kuhudumia wakimbizi
na waomba hifadhi kutoka Kongo walioko Tanzania si wajibu tu — ni taswira ya
ubinadamu wetu wa pamoja. Kupitia msaada madhubuti kutoka kwa washirika kama
Umoja wa Ulaya, hatutoi tu huduma za haraka, bali tunawekeza katika utu,
ustahimilivu, na misingi ya amani ya kudumu kwa familia zinazostahili matumaini
na mustakabali bora,” amesema Zulqarnain Hussain Anjum, Mwakilishi wa UNHCR
a.i. nchini Tanzania.
UNHCR inahitaji
takribani Dola za Kimarekani milioni 14 (sawa na TZS bilioni 37.8) kukabiliana
na dharura ya wakimbizi wa DRC nchini Tanzania, ikiwemo Dola milioni 5 (TZS
bilioni 13.5) kwa ajili ya maandalizi. Hivyo basi, shirika linaendelea kuomba
msaada zaidi kutoka kwa jumuiya ya kimataifa na wadau wa masuala ya kibinadamu.
Kufikia tarehe 31 Mei 2025, Tanzania ilikuwa inahifadhi wakimbizi zaidi ya
230,000, wengi wao kutoka Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
0 Maoni