Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la
Ngorongoro (NCAA) Dkt. Elirehema Doriye leo tarehe 12 Mei, 2025 amevisha vyeo
jumla ya watumishi 621 ikijumuisha Maafisa 145 na askari 476 wa jeshi la
Uhifadhi.
Akizungumza na watumishi hao baada ya kuwaapisha na
kuwavisha vyeo Dkt. Doriye amewasisitiza maafisa na askari wa jeshi la uhifadhi
kuzingatia kiapo walichoapa na kuzingatia maadili ya utendaji kazi, kuzingatia
sheria, ushirikiano, upendo na kujiepusha na rushwa katika maeneo ya kazi.
“Leo mmeapa na kuvishwa vyeo vya kijeshi, mnapaswa kuonesha
dhamira ya dhati ya kulinda Hifadhi ya Ngorongoro na rasilimali zote za
uhifadhi, vyeo mlivyovishwa vinakuja na majukumu makubwa ambayo yanahitaji
kujituma na kuwajibika ipasavyo, hakikisheni mnakuwa mfano bora kwa jamii kwa
kuzingatia maadili, nidhamu, sheria, uaminifu, uzalendo kwa rasilimali za nchi,
kujiepusha na vitendo vya rushwa na kufuata miongozo ya jeshi la Uhifadhi”
alisisitiza Dkt. Doriye.
Kamishna Doriye amewakumbusha watumishi hao kuwa, kupanda cheo ni
kuongezewa majukumu ya kiuongozi katika usimamizi wa shughuli za uhifadhi,
utalii, ulinzi, maendeleo ya jamii na urithi wa asili na utamaduni uliopo
hifadhi ya Ngorongoro na kusisitiza kuwa suala la mafunzo ya kijeshi kwa
watumishi wa NCAA litakuwa endelevu ili kuendelea kujenga utimamu wa mwili kwa
afisa na askari.
Awali akizungumza katika tukio hilo Kamishna Msaidizi
Mwandamizi wa Uhifadhi (SACC) anayesimamia Idara ya Rasilimali watu na Utawala
Salma Chisonga ameeleza kuwa tukio la kuvishwa vyeo watumishi hao ni
utekelezaji wa vibali vya kupandisha vyeo watumishi ambavyo vilitolewa na
Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, kwa
nyakati tofauti kati ya mwaka 2021/2022 hadi mwaka 2024/2025.
SACC Chisonga amebainisha kuwa maafisa 145 waliovishwa vyeo
wamegawanyika katika ngazi mbalimbali ambapo Maafisa uhifadhi Wakuu daraja la
kwanza ni 5, Maafisa uhifadhi Wakuu daraja la II ni 21, Maafisa uhifadhi
waandamizi ni 31, Maafisa uhifadhi daraja la I ni 56 na Mafiasa uhifadhi daraja
la II ni 32.
Ameongeza kuwa askari 476 waliovishwa vyeo wamegawanyika
katika ngazi mbalimbali ambapo askari wa uhifadhi mkuu daraja la I ni 39, askari wa uhifadhi wakuu daraja la II ni
54, askari wa uhifadhi Waandamizi ni 70, askari wa uhifadhi daraja la kwanza ni
86 na askari wa uhifadhi daraja la II ni 227.
0 Maoni