Katika jitihada za kukuza sekta ya utalii na kuimarisha shughuli za uhifadhi nchini, Serikali imeendelea kuboresha miundombinu ya mawasiliano katika maeneo ya Hifadhi za Taifa, hatua inayolenga kuhakikisha kuwa watalii wanapata huduma bora za mawasiliano wanapokuwa hifadhini, sambamba na kuwezesha shughuli za uhifadhi kufanyika kwa ufanisi zaidi kwa kutumia teknolojia ya kisasa.
Hayo yamesemwa jana Aprili
11, 2025 na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia Jerry Silaa wakati wa ziara
yake katika Hifadhi ya Taifa Mkomazi iliyopo mkoani Kilimanjaro kukagua na
kuhakikisha upatikanaji wa mitandao ya simu katika maeneo ya hifadhi hiyo na
vijiji jirani.
Waziri Silaa alisema kuwa “jumla
ya Minara 38 itajengwa katika mkoa wa Kilimanjaro ambapo Jumla ya Minara 6
itajengwa katika wilaya ya Mwanga kupitia mradi wa Tanzania ya Kidigitali, pia
kupitia timu ya wataalamu waliokuja kufanya utafiti tayari utambuzi wa eneo la
kuweka Mnara ambao utatumika kwa lango la Ndea la kuingilia Hifadhi ya Taifa
Mkomazi pamoja na maeneo mengine ya vijiji na kata za jirani
umeshafanyika”.
Kwa upande wake, Kamishna
Msaidizi wa Uhifadhi Emanuel Moirana ambaye ni Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Mkomazi
aliongeza kuwa upatikanaji wa mawasiliano ndani ya Hifadhi ya Taifa Mkomazi
utasaidia sana katika shughuli za utalii kwani watalii wataweza kuwasiliana
kirahisi na kushiriki katika usambazaji wa taarifa kuhusu hifadhi pamoja na
kurahisisha mawasiliano wakati wa shughuli za doria ndani ya hifadhi.
“Mawasiliano ni jambo muhimu
kwa wageni wetu, kunapokuwa na mtandao mzuri hifadhini watalii wataweza
kusambaza taarifa duniani kuhusu uzuri wa Mkomazi na pia kufanya shughuli
nyingine muhimu wakati wa safari zao za utalii, pia kama hifadhi itasaidia
katika utekelezaji na uendeshaji wa shughuli za doria,” alisema Kamishna
Moirana.
Naye, Diwani Kata ya Toroha
Palesio Nalio alisema kuwa upatikanaji wa mawasiliano katika hifadhi hiyo na
vijiji jirani utasaidia katika kutatua changamoto za migongano kati ya
wanyamapori na binadamu kwani utarahisisha
utolewaji wa taarifa pindi wananchi wanapoingiliwa na wanyama katika maeneo yao
hali itakayopelekea upatikanaji wa msaada kwa haraka.
Ziara ya Waziri wa
Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Jerry Silaa katika Hifadhi ya Taifa Mkomazi
ilikuwa na lengo la kutekeleza maelekezo ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa, ambayo alitoa tarehe 25 Machi, 2025 wakati
wa ufunguzi wa lango la Ndea na kusisitiza umuhimu wa upatikanaji wa huduma za
mawasiliano ya simu katika maeneo ya hifadhi hiyo.
Aidha, Waziri Silaa katika ziara yake aliambatana na viongozi mbalimbali kutoka Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari pamoja na uongozi wa Wilaya ya Mwanga wakiongozwa na Mkuu wa Wilaya hiyo Mwanahamisi Mukunda.
Na. Happiness Sam - Same
0 Maoni