Msoga, Chalinze - Ilikuwa ni
siku ya kihistoria na ya kipekee kabisa kijijini Msoga, jana Alhamisi Aprili 10,
2025, wakati Rais mstaafu Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete alipobeba Mwenge wa Uhuru
mbele ya mamia ya wananchi waliomiminika kushuhudia tukio hilo la kihistoria.
Mwenge wa Uhuru ulipowasili
rasmi mkoani Pwani, kijiji cha Msoga, hususan nyumbani kwa Rais huyo mstaafu kuligeuka
jukwaa la furaha, vigelegele na nyimbo za kizalendo. Kikwete, akiwa mwenye
bashasha na msisimko, alibeba mwenge huo kwa mikono miwili huku akiushikilia
kwa uhodari unaoashiria uzalendo na kumbukumbu ya safari ya ukombozi wa taifa.
Akizungumza kwa bashasha na
msisimko wa aina yake, Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete alisema:
“Ni furaha na heshima kubwa
kushiriki na wananchi wenzangu wa Msoga, kupokea Mwenge wa Uhuru kijijini
kwetu. Hili ni tukio la kihistoria na la kujivunia sana. Mwenge huu umebeba
ujumbe wa matumaini, mshikamano na maendeleo.”
Akaongeza kwa tabasamu:
“Hakika elimu haina mwisho.
Leo nimejifunza jambo muhimu sana—niliona vijana wa Kikosi cha Wakimbiza Mwenge
wakikagua ubora wa majengo ya Sekondari mpya ya Amali inayojengwa hapa kwetu
Msoga. Kilichonifurahisha zaidi ni namna walivyotumia vifaa na teknolojia ya
kisasa kabisa kufanya ukaguzi wao. Hawakubahatisha hata kidogo. Kila kitu
kilikuwa kwa viwango na taratibu!”
Rais mstaafu hakusita kutoa
pongezi kwa serikali ya sasa:
“Natoa pongezi nyingi kwa
Rais Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri na yenye tija anayoendelea kuifanya.
Kasi yake ya kuimarisha elimu, afya, miundombinu na maendeleo ya kijiji kama
Msoga ni ya kuigwa. Hili ni Taifa letu sote—na linapokua, nasi tunakua pamoja
nalo.”
Alimaliza kwa kuhimiza
vijana wa Msoga na Tanzania kwa ujumla kuendelea kuthamini Mwenge wa Uhuru kama
ishara ya umoja, uzalendo na maendeleo yanayogusa maisha
ya kila Mtanzania.
0 Maoni