WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa leo Machi 13, 2025 amezindua
kituo kipya cha Mabasi cha Nzega mjini ambacho ujenzi wake umegharimu shilingi
bilioni 4.327.
Akizungumza baada ya kuzindua kituo hicho ambacho utekelezaji wake umefikia asilimia 100, Mheshimiwa Majaliwa ameipongeza halmashauri hiyo kwa uamuzi wa ujenzi wa kituo hicho kwani kitaibua fursa za biashara kwa wakazi wa eneo hilo.
“Kituo hiki ni kizuri na kimejengwa kwa ubora, kituo hiki
kinatakiwa kianze kutumika ili wananchi waanze kunufaika nacho, Watumishi wa
halmashauri ongozeni Wana-Nzega kunufaika na fursa katika eneo lenu.”
Aidha, Mheshimiwa Majaliwa ametoa wito kwa halmashauri hiyo
kuongeza vibanda vya wafanyabiashara badala ya vichache ambavyo vimejengwa
mpaka sasa. “Tunataka wananchi wengi zaidi wanufaike, ongezeni vibanda, huu ni
ubunifu mzuri sana utasababisha wengi wanufaike, waleteni wajasiriamali hapa
wapate rizki zao, mkifanya hivyo mtaongeza mzunguko wa fedha.”
Kadhalika, Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa Serikali
inaendelea na mpango kazi wake wa kuwahudumia watanzania wakati wote, “Serikali
hii ya Chama cha Mapinduzi inaendelea kukamilisha malengo yake katika
kuwatumikia watanzania ninajua hatua tuliyoifikia.”
Katika hatua nyingine, Mhehimiwa Majaliwa ametoa wito kwa watumishi wa halmashauri nchini kuendelea kujielekeza katika kutatua changamoto za wananchi “Tumueni mapato yenu ya ndani kutekeleza miradi.”




0 Maoni