Waziri wa Maendeleo ya Kimataifa wa Canada Mh. Ahmed Hussein
na Waziri wa Madini wa Tanzania Mh. Anthony Mavunde wamefanya mazungumzo ya
masuala mbalimbali ya kuboresha uhusiano baina ya nchi mbili hizo hasa katika
eneo la kuwajengea uwezo wataalamu na wachimbaji wa madini nchini Tanzania
katika matumizi ya teknolojia ya kisasa ya uchimbaji na uchenjuaji madini.
Mazungumzo hayo yamefanyika jana Toronto, Canada na
kuhudhuriwa na Balozi wa Tanzania nchini Canada Mh. Joseph Sokoine sambamba na
wataalamu wa Wizara zote mbili.
Akitoa maelezo ya awali, Waziri Ahmed Hussein ameipongeza
Tanzania chini ya uongozi wa Mh. Rais Dkt. Samia S. Hassan kwa namba ambayo
imeweka mazingira mazuri ya ukuaji wa sekta ya Madini nchini na kwamba Canada
itaendelea kuimarisha uhusiano wake na Tanzania hasa katika eneo la kuwajengea
uwezo wataalamu na wachimbaji madini kwenye matumizi sahihi ya teknolojia ya
uchimbaji na uchenjuaji madini.
“Tumekuwa na miradi ya maendeleo ya elimu nchini
Tamzania,hivyo kupitia vyuo vya mafunzo ya Ufundi itakuwa rahisi kuja na
mafunzo maalum ya kuwajengea uwezo wananchi wa Tanzania,hasa wakina mama na
vijana, kushiriki kikamilifu kwenye mnyororo mzima wa sekta ya madini,” alisema
Hussein.
Kwa upande wake,Waziri Anthony Mavunde ameishukuru nchi ya
Canada kwa ushirikiano mkubwa inaoutoa katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii
nchini Tanzania na pia kubainisha uwepo wa Kampuni kubwa za Madini kutokea
nchini Canada zimechochea kwa kiwango kikubwa maendeleo ya kiuchumi kupitia
fursa mbalimbali zitokanazo na uwekezaji huo.
“Tanzania hivi sasa tuna programu yenye lengo la kuwezesha
ushiriki kamilifu wa wakinamama na Vijana kwenye sekta ya madini,hivyo
kuwajengea uwezo wa kiujuzi kwenye mnyororo mzima wa thamani wa sekta ya madini
kutachochea kukua kwa kasi kwa sekta ya madini.
Vyuo vya Mafunzo ya Ufundi vinaweza kutumika kutoa mafunzo
maalum ya jamii husika kutokana na aina ya shughuli za madini katika eneo
husika.
“Tanzania itatoa ushirikiano wa kutosha kwa Canada katika
utelekezaji wa mpango huu wenye tija kwa nguvu kazi ya Taifa Tanzania,” alisema
Mavunde.
Akitoa maelezo ya ziada,Balozi Joseph Sokoine ameikaribisha mifuko ya Hifadhi ya Jamii nchini Canada kuwekeza nchini Tanzania kwenye maeneo mbalimbali ikiwemo eneo la ujenzi wa miundombinu na kwenye sekta ya madini.



0 Maoni