Wabunge wa
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii wameishauri Mamlaka ya
Hifadhi ya eneo la Ngorongoro (NCAA) kuendelea kubuni mazao mapya ya utalii
katika mapango ya Amboni yaliyopo mkoani Tanga ili kutoa fursa kwa wageni wengi
zaidi kutembelea kivutio hicho ambacho ni urithi wa mambo kale.
Akitoa
maelekezo ya kamati hiyo kwa wizara ya Maliasili na Utalii mara baada ya ziara
ya kikazi katika mapango hayo mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi,
Maliasili na Utalii mheshimiwa Timotheo Mnzava amesema kuwa eneo hilo lina
fursa nyingi la mazao mapya ya utalii hivyo ni jukumu la wizara na NCAA kukaa
chini na kuona jinsi ya kuboresha mazingira ya mapango ya Amboni yawe ya
kipekee na kuvutia zaidi.
“Nazungumza
kwa niaba ya waheshimiwa wabunge ambao leo wametembelea eneo hili na kujionea
kazi kubwa mnayoifanya katika kukuza utalii, ni jukumu lenu sasa kuhakikisha
licha ya uwepo wa mapango haya lakini pia mnafanya kila jitihada kuwa na mazao
mapya ya utaalii kwa kuwa eneo hili ni kubwa na linaruhusu shughuli nyingi za
utalii,” alisema mheshimiwa Mnzava.
Kwa upande
wake Waziri wa Maliasili na Utalii mheshimiwa Balozi Dkt. Pindi Chana
aliwaeleza wabunge hao kuwa wizara yake itaendelea kusimamia maelekezo yote
yanayotolewa na kamati ili kuhakikisha kuwa kila chanzo cha utalii
kinachoanzishwa kinakuwa na tija kwa taifa.
Balozi Chana
ameeleza kuwa wizara yake iliamua kukabidhi mapango hayo kwa Mamlaka ya Hifadhi
ya Ngorongoro kwa ajili ya kuboresha uhifadhi, na kuyatangaza zaidi ili kuongeza idadi ya watalii wa ndani
na nje ya Nchi.
Kwa upande
wake Kamishna wa uhifadhi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro Dkt. Elirehema
Doriye aliwaambia wabunge wa kamati
hiyo kuwa mamlaka imejipanga kuboresha
eneo hilo kwa kuanzisha mazao mapya ya utalii ikiwemo makumbusho ya viumbe wa
baharini, maeneo ya kupumzikia, mchezo wa kutembea na kamba “zip line” pamoja
na huduma za nyingine za kijamii na kitalii katika eneo la mapango.
Ziara hiyo
pia ilihudhuriwa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii mheshimiwa Dunstan
Kitandula (Mb) Naibu Katibu Mkuu wizara hiyo anayesimamia Uhifadhi CP Benedict Wakulyamba, menejimenti ya mamlaka
ya Hifadhi ya Ngorongoro na watendaji wa wizara ya Maliasili na Utalii.
0 Maoni