TARURA yaendelea kuondoa vikwazo katika barabara wilayani Nzega

Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) inaendelea kuboresha barabara za vijijini kupitia mradi wa RISE sehemu ya uondoaji vikwazo katika barabara hususani maeneo ya vijijini.

Akiongea katika mahojiano maalum, Meneja wa TARURA Wilaya ya Nzega, Mhandisi Sumbuko Twaha amesema kuwa uondoaji wa vikwazo katika Barabara unalenga kuwawezesha wananchi kusafirisha mazao yao kwa urahisi na kuzifikia huduma za kijamii.

"Tuliamua kujenga mradi huu wa boksi kalavati lenye urefu wa mita 12 katika barabara ya Ijanija-Butandula-Uchama ili kuhakikisha wananchi wanasafiri kwa urahisi kwani hapo mwanzo ilikuwa vigumu kwa wananchi kuvuka eneo hili," amesema.

Naye, Christopher Richard mkazi wa Wilaya ya Nzega, amesema kuwa wananchi wa kijiji cha Butandula walikuwa wanapata shida ya usafiri hasa wakati wa masika lakini sasa wanaishukuru serikali kwa kuwajengea kalavati kwani wanasafiri bila shida kufikia huduma za kijamii.

Kwaupande wake, Richard Thomas ambaye pia ni mkazi wa Nzega amesema kuwa mradi huo umekuwa mkombozi hasa baada ya maeneo korofi kuanza kupitika katika Wilaya hiyo.

"Tunaishukuru Serikali kwa mradi huu ambao umekuwa mkombozi kwa wananchi maana hapo mwanzo ilikua vigumu kwa wananchi kusafiri na hata kusafirisha mazao yao," amesema.

Mradi wa uondoaji vikwazo katika barabara unatekelezwa na Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kupitia mradi wa RISE na unagharamiwa na mkopo nafuu kutoka Benki ya Dunia.



Chapisha Maoni

0 Maoni