WAZIRI MKUU,
Kassim Majaliwa ameiagiza Idara ya Menejimenti ya Maafa na Jeshi la Zimamoto
kutumia mapendekezo yaliyomo kwenye tafiti ya marehemu Billy Mwakatage ambaye
ni mhitimu wa shahada ya Uzamivu (PhD) aliyefanya tafiti kuhusu majanga ya moto
kwenye masoko ya umma.
Ametoa wito
huo jana Desemba 05, 2024, alipomwakilisha Makamu wa Rais Dkt. Philip Isdor
Mpango kwenye mahafali ya 43 ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania yaliyofanyika
katika viwanja vya Kawawa, Manispaa ya Kigoma. Shahada hiyo ilipokelewa na
Mjane wa Marehemu Bi. Ningile Kapange.
Amesema kuwa
tafiti hiyo ina mahusiano makubwa na shughuli inayofanywa na Ofisi ya Waziri
Mkuu kupitia Idara ya Maafa katika kudhibiti maafa na majanga mbalimbali.
“Kwa kuwa
ameshahitimu na leo anapata shahada na amefanya utafiti wa kina kwenye eneo
hili la maafa na hasa majanga ya moto ambayo wakati wote Serikali tumekuwa
tukipambana nayo, msomi wetu Marehemu Billy Mwakatage pamoja na utafiti ametoa
mapendekezo mbalimbali, chukue utafiti huu na muufanyie kazi katika kukabiliana
na majanga hapa nchini.”
Tafiti ya
Marehemu Billy Mwakatage alifanya tafiti kuhusu “mambo yanayoathiri na nia ya
kuzuia milipuko ya moto katika soko la umma nchini Tanzania.”
Katika hatua
nyingine Mheshimiwa Majaliwa ameiagiza Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
kuandaa mpango wa mafunzo kwa wahadhiri nchini ili wapate fursa za kufanya
tafiti kwa kushirikiana na wenzao kutoka sehemu mbalimbali duniani.
Pia,
ameiagiza Wizara hiyo kuandaa mpango mahsusi wa kukuza kazi za ubunifu na iweke
mkakati wa kuwezesha kuuza bunifu hizo. “Kama mnavyofahamu ubunifu ni biashara.
Pia, ubunifu unazalisha ajira na kuongeza kasi yamaendeleo ya Taifa.”
0 Maoni