Umoja wa
Ulaya (EU) na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar wamesaini makubaliano mawili
muhimu yanayolenga kukuza maendeleo endelevu, uhifadhi wa bahari, na usawa wa
kijinsia.
Makubaliano
hayo yalisainiwa mbele ya Mhe. Riziki Pembe Juma, Waziri wa Maendeleo ya Jamii,
Jinsia, Wazee na Watoto; Rita Laranjinha, Mkurugenzi Mtendaji wa Masuala ya
Afrika wa Huduma za Nje za Umoja wa Ulaya; na Hans Stausboll, Kaimu Mkurugenzi
wa Kamisheni ya Umoja wa Ulaya Kanda ya Afrika, pamoja na maafisa waandamizi wa
serikali na wadau wa maendeleo.
Makubaliano
ya kwanza, yenye thamani ya TZS bilioni 32 (€ milioni 11), yanahusu uhifadhi wa
bahari kupitia Mradi wa Bahari Yetu. Mradi huu, unaotekelezwa na Shirika la
Kimataifa la Uhifadhi wa Mazingira (IUCN), unalenga kushughulikia changamoto
muhimu za kulinda rasilimali za bahari, kukuza uvuvi endelevu, na kupambana na
uchafuzi wa plastiki. Aidha, mradi huu utaziwezesha jamii za Zanzibar kiuchumi
kwa kuanzisha fursa za maendeleo endelevu huku ukihifadhi bioanuwai tajiri ya
bahari ya Zanzibar.
Makubaliano
ya pili yanatenga TZS bilioni 8.8 (€ milioni 3) kupitia mpango wa Umoja wa
Ulaya wa Gender Transformative Action Zanzibar, unaotekelezwa na UN Women kwa
kushirikiana na wizara inayohusika na masuala ya jinsia Zanzibar. Mpango huu
unalenga kuondoa vikwazo dhidi ya haki za wanawake na kuimarisha nafasi za
uongozi wa wanawake katika sekta za umma na binafsi. Aidha, mkazo mpya utawekwa
kwenye kukuza elimu ya wasichana, hususan elimu ya juu.
Akizungumza
wakati wa hafla hiyo, Bi. Laranjinha alisema: “Makubaliano haya yanaonyesha
dhamira ya Umoja wa Ulaya katika kuleta maendeleo Zanzibar, hususan katika
sekta za uchumi wa buluu na kuimarisha usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa
wanawake.”
Kwa upande
wake, Bw. Stausboll aliongeza: “Makubaliano haya ni ushuhuda wa dhamira ya
Umoja wa Ulaya ya kuleta manufaa na maendeleo ya kudumu kisiwani Zanzibar.
Miradi hii italeta ustawi wa pamoja,, na ujumuishaji wa kijamii.”
Awali,
Laranjinha na Stausboll walifanya mazungumzo na Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Mwinyi,
kabla ya kushiriki hafla ya utiaji saini. Mnamo tarehe 10 Desemba, wanatarajiwa
kushiriki katika Mazungumzo ya Ushirikiano kati ya Umoja wa Ulaya na Serikali
ya Tanzania, hatua inayotegemea kuimarisha ushirikiano wa muda mrefu na
kushughulikia vipaumbele vya pamoja vya pande zote mbili.
0 Maoni