Waziri Silaa awaasa waandishi wa habari kuelekea uchaguzi

 

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Jerry Silaa amewataka waandishi wa habari kuzingatia kanuni, sheria na maadili ya uandishi wa habari wakati wakiripoti habari za uchaguzi wa Serikali za Mitaa pamoja na Uchaguzi Mkuu utakaofanyika mwakani.

Mh. Silaa ametoa kauli hiyo leo Jijini Dar es Salaam katika  Mkutano wa Wadau wa Sekta ya Habari Kuelekea Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024 na Uchaguzi Mkuu 2025 uliohudhuriwa pia na Makamanda wa Jeshi la Polisi wa mikoa yote nchini.

Mhe. Silaa amesema kwamba vyombo vya habari vinawajibu wa kuwahabarisha wananchi kuhusiana na uchaguzi kwa kuhakikisha kuwa vinatenda haki ya kutoa habari za uhakika na zilizochakatwa kwa weledi mkubwa.

Amesema kuwa wizara yake inatambua mchango unaotolewa na vyombo vya habari kwa kutoa habari mbalimbali za miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali, na kuahidi kuwa yeye yupo tayari kutoa ushirikiano wa kutosha kwa vyombo vya habari.

Mhe. Silaa ameeleza kuwa kutokana na kuboreshwa kwa mazingira rafiki ya vyombo vya habari nchini hadi sasa, Tanzania ina jumla ya magazeti 179, Majarida 174, Radio 247, Mitandaoni 355 pamoja na Runinga 68 zilizosajiliwa.

Kwa upande wake Msemaji wa Jeshi la Polisi David Misiime amesema kuwa kuna umuhimu wa vyombo vya habari kufanya kazi kwa ushirikiano katika matukio mbalimbali yakiwemo ya uchaguzi ili kuepusha migongano wakati wa kutekeleza majukumu yao.

“Ni muhimu polisi kutambua na kuheshimu mipaka ya kitaaluma ya waandishi wa habari na vivyo hivyo kwa waandishi wa habari kuheshimu mipaka ya kitaaluma ya polisi wakati wakitekeleza majukumu yao,” alisema Kamanda Misiime.

Chapisha Maoni

0 Maoni