Baadhi ya wananchi wa Cuba waliotembelea banda la Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro katika tamasha la kimataifa la Kiswahili wameeleza kufurahishwa kwao kutokana na kupata taarifa mbalimbali zinazohusu vivutio vya Tanzania ikiwemo hifadhi ya Ngorongoro.
Wakizungumza
kwa nyakati tofauti katika banda hilo baadhi ya watu kutoka Cuba waliotembelea
banda hilo wamesema wamekuwa wakiiona hifadhi hiyo kupitia picha mbalimbali
ikiwemo filamu ya The Royal Tour iliyoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan.
“Tunavutiwa
na juhudi hizi za kuutangaza utalii wenu katika nchi hizi za Karibe,tunaiona
Ngorongoro kupitia picha na makala mbalimbali mitandaoni,natamani siku moja
kufika Ngorongoro,” alisema Alejendro Alex mmoja wa wanafunzi wa Chuo Kikuu cha
Havana cha jijini Cuba.
Naye Marie
Alexndrea kutoka taasisi ya utangazaji wa utalii nchini Cuba alipongeza
jitihada kubwa zinazofanywa na watanzania katika kutangaza vivutio vyao vya
utalii kwa mataifa mengine ambapo alieleza kuwa kitendo hicho kinasaidia
kuonesha ni kwa jinsi gani watu wengi duniani watakavyoweza kuvijua vivutio
hivyo.
“Hii
inapendeza, tumemuona hata Rais wenu akifanya kazi kubwa ya kutangaza
utalii,bila shaka kadri mtakavyotangaza vivutio vyenu katika ukanda huu wa
karibe itasaidia pia kuongeza idadi ya watalii katika hifadhi ya Ngorongoro na
Tanzania kwa ujumla,”alisema Marie.
Balozi wa
Tanzania nchini Cuba mheshimiwa Humphrey Polepole pembezoni mwa mkutano huo
aliipongeza Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kwa uamuzi wake wa kushiriki
tamasha hilo na kusema kuwa yupo mbioni kuandaa mkakati mahsusi katika kuandaa
mpango wa kutangaza utalii katika maeneo mbalimbali ya ukanda wa karibe.

0 Maoni