Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), limeeleza kutofurahishwa na mwendelezo wa Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Jerry Silaa kukwepa mialiko ya mikutano inayoandaliwa na wadau wa habari.
Akizungumza
katika ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Nane TEF leo tarehe 7 Novemba 2024, Mwenyekiti
wa TEF Deodatus Balile amesema, waziri huyo tangu ateuliwe na Rais Samia Suluhu
Hassan tarehe 22 Julai 2024, amealikwa katika matukio ya kihabari minne ikiwemo
huu TEF, yote hajahudhuria.
“Waziri wetu
huyu, sisi hatuna mambo ya kusema chini chini maana sisi tukisema chini chini
wengine watafanyaje? Amealikwa kwenye mkutano wa wadau wa habari Arusha PRST
hakwenda,” amesema Balile.
Balile
ameongeza kwa kusema kuwa “Amealikwa kwenye Tuzo za Uandishi wa Habari Mahiri
(EJAT), hakwenda. Nikasikia amealikwa Mbeya, tukasema basi (sisi TEF) tumpe
nafasi akutane na sisi tumualike, hakuja anasema Spika amemzuia.”
Pamoja na
mambo mengine, Balile amempongeza Waziri Silaa kwa kuteua bodi ya ithibati ya
wanahabari itakayofuatiwa na hatua ya kuundwa kwa baraza la habari ambalo litasaidia
kuepusha waandishi wa habari kushtakiwa mahakamani.
Pia, amemuomba Waziri Silaa kuongea na mawaziri wenzake na kuwashauri kuwa na utaratibu wa kukutana na waandishi wa habari kuelezea mambo mbalimbali zinazofanywa na wizara zao ili zifahamike na wananchi.

0 Maoni