Mkuu wa Misheni ya Uangalizi wa Uchaguzi ya SADC (SEOM)
katika Uchaguzi Mkuu wa Mauritius Mhe. Jaji (Mstaafu) Mohammed Chande Othman,
amezindua misheni hiyo jijini Port-Louis, Mauritius, kwa niaba ya Mwenyekiti wa
Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan. Uzinduzi huo uliofanyikia kwenye Kituo
cha Sanaa cha Caudan, pia umewaaga waangalizi wa uchaguzi 35 ambao wameondoka
kwenda maeneo tofauti kwa ajili ya kazi hiyo.
Katika hotuba yake, Mheshimiwa Chande alibainisha kuwa
dhumuni kuu la misheni hiyo ni kufanya tathmini ya mwenendo wa uchaguzi nchini
Mauritius kwa kuzingatia katiba na kanuni za uchaguzi za nchi hiyo, pamoja
na misingi iliyowekwa katika Kanuni na Miongozo ya SADC inayosimamia Uchaguzi wa
Kidemokrasia. "Dhamira yetu siyo tu kuangalia uchaguzi, bali ni kuchangia
kwa njia ya kujenga, huku tukifanya tathmini ya kina kama uchaguzi unazingatia
viwango vya kidemokrasia," alisema Mheshimiwa Chande.
Akizungumza mbele ya wadau mbalimbali waliofika kwenye
uzinduzi huo ikiwemo Jumuiya ya Wanadiplomasia, Mhe. Chande alitambua kazi
kubwa inayofanywa na SADC katika kusimamia chaguzi kwenye ukanda wa Kusini mwa
Bara la Afrika ambapo alieleza kuwa uchaguzi wa Mauritius ni sehemu ya mfululizo
wachaguzi kwenye nchi wanachama saba wa SADC wenye takribani raia milioni 130,
taswira anayoakisi dhamira ya jumuiya ya kuimarisha mabadiliko ya kidemokrasia.
SEOM, ambayo ilianza kazi zake za maandalizi ya usimamizi wa
uchaguzi nchini humo mnamo tarehe 28 Oktoba, inajumuisha waangalizi 73, kutoka
nchi nane wanachama wa SADC. Timu yaa waangalizi 35 iliyobobea kwenye masuala ya
uangalizi wa chaguzi itapelekwa kwenye majimbo yote ya uchaguzi ambapo
wataangalia masuala mazima ya maandalizi kabla ya uchaguzi, taratibu za siku ya
uchaguzi, na shughuli baada ya uchaguzi. Vigezo muhimu vya uangalizi ni pamoja
na uhuru wa wananchi kujieleza, upatikanaji wa vituo vya kupigia kura, muda wa
kufunguliwa na kufungwa kwa vituo vya kupigia kura, elimu ya wapiga kura, na
haki ya taasisi za uchaguzi. Mheshimiwa Chande alisisitiza kuwa mambo haya ni
muhimu katika kuhakikisha kuwa uchaguzi sio tu unafuata taratibu, bali pia
unakidhi matarajio ya kidemokrasia ya wananchi wa Mauritius.
Akijibu maswali ya waandishi wa Habari, Mheshimiwa Chande alisifu
wananchi wa Mauritius kwa kuwa na imani kubwa na vyombo vyao vya kuendesha
uchaguzi. Alisisitiza kuwa ni nchi chache sana barani Afrika ambazo zina idadi
kubwa ya wapiga kura, lakini pia kufanikisha kuwasajili kwa asilimia 98 kwenye
daftari la wapiga kura. Alisema hii ni hatua kubwa sana ya demokrasia
nchini humo, na inahamasisha wananchi wengine barani Afrika kufuata nyayo hizo
na kutimiza haki ya kikatiba.
Hivyo aliwasihi wadau wote, ikiwemo vyama vya siasa, asasi
za kiraia, na vyombo vya habari, kuendesha shughuli zao kwa amani ili uchaguzi
huo ufanyike katika mazingira ya amani. Aliwahimiza wananchi wa Mauritius
kujitokeza kwa wingi kama walivyojiandikisha, kutumia haki zao za kikatiba na
kutimiza demokrasia kwa kupigakura na kuheshimu matokeo ya uchaguzi, ambayo
SEOM itayaangalia kwa ukaribu. Taarifa ya awali ya matokeo ya uangalizi wa SEOM
itatolewa tarehe 12 Novemba 2024, siku mbili baada ya kupigwa kura tarehe 10
Novemba, 2024.
Wajumbe wa Misheni ya Uangalizi wa Uchaguzi ya SADC nchini Mauritius ina wajumbe wapatao 73 kutoka nchi nane (8) za Wanachama wa SADC ambazo ni Jamhuri ya Botswana, Mozambique, Namibia, Afrika Kusini, Zambia na Zimbabwe, Ufalme wa Eswatini na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Waangalizi hao wa uchaguzi walipitia mafunzo ya siku nne kuanzia tarehe 1 hadi 4 Novemba 2024, ili kupata ufahamu na muktadha wa uchaguzi nchini Mauritius. Waangalizi hao watapelekwa katika wilaya kumi za utawala za Mauritius, ambazo ni, Black River, Flacq, Grand Port, Moka, Pamplemousses, Plaines-Wilhems, Port-Louis, Rivière du Rempart, Savanne na Rodrigues.



0 Maoni