WAZIRI MKUU,
Kassim Majaliwa amesema kuwa matumizi ya mfumo wa kielektroniki wa Baraza la
Mawaziri utasaidia kuboresha utendaji kazi na kuleta ufanisi zaidi katika
kuwahudumia wananchi.
Amesema kuwa
maboresho hayo ya matumizi ya mfumo wa kielektroniki yatasaidia kwa kiasi
kikubwa kupunguza matumizi ya karatasi katika vikao vya Serikali, hususan
Baraza la Mawaziri, hivyo kupunguza changamoto ikiwemo kuchelewa kwa taarifa,
gharama kubwa za uchapaji na hatari ya upotevu wa taarifa muhimu.
Amesema hayo
leo (Jumatatu, Novemba 11, 2024) wakati akifunga Mkutano wa Kazi wa Mawaziri na
Naibu Mawaziri kuhusu matumizi ya mfumo wa kielektroniki wa Baraza La Mawaziri
(e-CABINET), kwenye ukumbi wa Hazina jijini Dodoma.
Ameongeza
kuwa hatua hiyo inatokana na jitihada na malengo ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia
Suluhu Hassan ya kusisitiza umuhimu wa Mawaziri na watumishi wa umma kuzingatia
mabadiliko ya kiteknolojia katika utendaji kazi.
“Matokeo ya
mwaka 2023 ya ulinganifu baina ya nchi katika muktadha wa Ukomavu wa Matumizi
ya Teknolojia Serikalini (Government Technical Maturity Index), nchi yetu
ilishika nafasi ya tatu (3) ikilinganishwa na nchi nyingine Barani Afrika.
"Tunampongeza na kumtakia kila la kheri Rais Dkt. Samia aendelee kubuni zaidi
kwa manufaa ya Taifa letu. ”
Kadhalika,
Waziri Mkuu amesema kuwa mkutano huo kuhusu matumizi ya mfumo wa kielektroniki
wa Baraza la Mawaziri ni sehemu ya juhudi za serikali katika kuhakikisha kwamba
Mawaziri na watumishi wa umma wanakuwa na ujuzi wa kisasa wa uendeshaji wa
shughuli za Serikali na utumishi kwa ujumla.
Wakati
huohuo, Waziri Mkuu amesema kuwa uanzishwaji wa mfumo huo wa kielektroniki wa
Baraza la Mawaziri ni utekelezaji wa Ibara za 102 na 103 za Ilani ya Uchaguzi
ya CCM ya Mwaka 2020 zinazoelekeza Serikali kuhakikisha kuwa sayansi,
teknolojia na ubunifu vinatumika kikamilifu katika kuendesha sekta za kukuza
uchumi kwa lengo la kufikia uchumi wa hadhi ya kipato cha kati ambao ni
shindani, jumuishi na unaoongozwa na viwanda.
Kwa Upande
wake, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dkt. Doto Biteko amewapongeza
wataalam kutoka Wakala wa Serikali Mtandao kwa kufanikisha mafunzo hayo.
“Tunaamini tumeelewa kwa kiwango kikubwa sana. ”
Naye, Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora,
Mheshimiwa George Simbachawene amesema kuwa mafunzo hayo ni mwendelezo wa
mpango wa Serikali kwenda kwenye matumizi ya mfumo wa kielektroniki wa Baraza
La Mawaziri (e-CABINET) mchakato ambao ulikuwa wa muda mrefu kupitia wataalam
wa Wakala wa Serikali Mtandao.



0 Maoni