Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Doto Mashaka
Biteko ameipongeza Wizara ya Madini kwa mkakati wanaoutekeleza ambao unawazesha
upatikanaji wa akiba ya Dhahabu kupitia Benki kuu ya Tanzania jambo ambalo ni
muhimu kwa maendeleo ya Uchumi wa Tanzania.
Hayo yamesemwa jana Oktoba 05 2024 wakati wa ufunguzi wa maonesho ya saba ya Kitaifa ya Teknolojia ya Madini yenye kauli mbiu ya “Matumizi ya Teknolojia sahihi ya Nishati safi katika sekta ya Madini kwa maendeleo endelevu” yanayofanyika Mkoani Geita.
“Sisi utajiri ambao Mungu ametujaalia ni utajiri wa madini
ikiwemo Dhahabu, lazima madini haya yawe chachu katika ukuaji wa uchumi wetu. Naipongeza
Wizara ya Madini kwa bidii kubwa mlioifanya sasa ya kuanzisha na kusukuma uwepo
wa akiba ya Dhahabu kupitia Benki kuu ya Tanzania,”alisema Mh. Biteko.
Kwa upande wake Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde
ameeleza kwamba kwa sasa baada ya kukaa pamoja baina ya serikali na wadau
wamefikia muafaka na hakuna mgomo tena wa kutoiuzia Dhahabu BOT baada ya
ufafanuzi wa baadhi ya hoja na elimu kutolewa ikiwa ni sehemu ya falsafa ya
maridhiano inayohubiriwa kwa nguvu na Mh Rais Dkt. Samia S. Hassan.
Mh Mavunde ametoa rai kwa wadau wote kushirikiana na
serikali katika mpango huu wa upatikanaji wa akiba ya dhahabu kupitia BOT na
kuahidi kutoa ushirikiano katika kushughulikia changamoto mbalimbali
zitakazojitokeza.
Akitoa maelezo ya awali, Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhe. Martin
Shigela ameipongeza Serikali kwa jitihada zake za kukuza Sekta ya Madini hasa
kwa Wachimbaji wadogo na kuahidi kwamba Mkoa wa Geita utaendelea kuwa chachu ya
ukuaji wa uchumi kupitia sekta ya madini ambapo mkoa huo ni mzalishaji mkubwa
wa madini ya dhahabu.
Naye Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya ya Bunge ya
Nishati na Madini Mhe. Kilumbe Shabani Ng’enda ameeleza kuwa Kamati inaridhishwa
na mwenendo wa Wizara ya madini hususani inavyosimamia sheria na sera ya madini
kwa manufaa ya uchumi wa watu na nchi kwa ujumla.
Akitoa salamu zake,Rais wa Shirikisho la Vyama cha Wachimbaji Madini(FEMATA) Ndg. John W. Bina ameipongeza Wizara ya madini kwa usikivu na majadiliano ya mara kwa mara pindi changamoto zinapojitokeza na kuahidi kwamba baada ya kikao cha pamoja wadau wameridhia mpango wa serikali wa ununuzi wa dhahabu kupitia BOT.
0 Maoni