Mastaa kutoka China wakiwemo nguli wa televisheni, filamu na
muziki wametua leo jijini Arusha kuelekea Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na
maeneo mengine ya nchi kurekodi moja ya vipindi vinavyotazamwa zaidi nchini
humo cha televisheni kiitwacho “Divas Hit the Road.”
Katika kipindi hicho, mastaa hao hutakiwa, kama ilivyokuwa kwenye mtindo wa filamu ya
“Royal Tour” aliyoshiriki Mhe Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuishi maisha ya
kawaida wakiwa bila ya walinzi wala wasaidizi wao wakitembelea nchi mbalimbali
duniani ambapo kwa Afrika Tanzania itakuwa nchi ya tatu baada ya Afrika Kusini
na Namibia.
Akiwapokea wageni hao kwenye Uwanja wa Ndege wa Arusha leo
Jumamosi Agosti 10, 2024, wakitokea Zanzibar walikoanzia kurekodi kipindi
hicho, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi,
amesema ujio wa mastaa hao utasaidia mkakati wa kuitangaza zaidi nchi yetu
katika soko la utalii, biashara na uwekezaji nchini China na duniani kwa
ujumla.
“Kama mnavyojua mwaka huu Mhe. Rais wetu Dkt. Samia Suluhu
Hassan alianzisha mkakati wa kujitangaza China kwa kurekodi filamu maalum kwa
soko la nchi hiyo iitwayo “Meilii Tansaniya” (Amazing Tanzania) pamoja na staa
wa filamu wa China Jin Dong. Ujio wa madiva hawa leo ni mwendelezo wa mkakati
huo,” alisema Dkt. Abbasi na kuongeza kuwa Waziri wa Utalii, Mhe. Angellah
Kairuki, pia atashiriki kwenye kipindi hicho Agosti 12 mwaka huu.
Kipindi cha “Divas Hit the Road” huoneshwa katika kituo cha
televisheni maarufu ya nchini China cha Hunan TV na hukadiriwa kutazamwa na
watu zaidi ya milioni 220 kwenye TV huku kikifuatiliwa na watu takribani
bilioni 3.07 kupitia mitandao mbalimbali ya kijamii ndani na nje ya China.
Aidha, kipindi hicho kimepata tuzo za kutajwa kuwa moja ya
vipindi bora vya masuala ya safari (the top traveling show in China) na pia
kutajwa kama alama ya vipindi vinavyoonesha uhalisia wa maisha (the new
benchmark of reality shows).
Pamoja na wapigapicha na waandaaji wengine wanaofika 100
waliofika nchini kuandaa kipindi hicho, mastaa saba waliokuja kutoka tasnia za
televisheni, filamu na muziki kwa ujumla wanawafikia watu zaidi ya milioni 500
kupitia mitandao yao mbalimbali ya kijamii akiwemo mwimbaji mashuhuri nchini
humo Song Qian mwenye wafuasi milioni 46 kwenye mtandao wa kijamii wa Weibo
pekee.
Kipindi cha Tanzania kinatarajiwa kurushwa Disemba mwaka huu wakati wa majira ya Sikukuu ya Krismas sambamba na vipindi vya nchi nyingine za Chile na Ufaransa.
0 Maoni