WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali ya awamu ya
sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea
kuthamini na kutambua mchango wa sekta binafsi katika kuimarisha ustawi wa
jamii ya Watanzania.
Ameyasema hayo leo (Jumapili, Februari 18, 2024)
alipomuwakilisha Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kufungua hospitali ya
Saifee Tanzania jijini Dar es Salaam. Amesema sekta binafsi zimekuwa zikiunga
mkono jitihada za Serikali katika kutoa huduma mbalimbali kwa wananchi.
Waziri Mkuu amesema mchango wa sekta binafsi katika eneo la
kutoa huduma kwa wananchi ni mkubwa na unadhihirika kupitia huduma mbalimbali wanazozitoa
ambazo ni pamoja na huduma za afya, elimu, mawasiliano na maji.
Amesema kwa upande wa sekta ya Afya, Serikali inatekeleza
kwa vitendo Sera ya Ubia kwa kufanya kazi pamoja na baadhi ya vituo vya kutolea
huduma ya afya vinavyomilikiwa na sekta binafsi.
Pia, Waziri Mkuu amesema amefarijika na huduma zinazotolewa
na hospitali hiyo zikiwemo za upasuaji wa moyo, mgongo, ubongo kwa kutumia
teknolojia za kisasa za kitabibu na pia kuweka vipandikizi (implants) kwenye
matibabu ya mifupa.
“Ni matumaini yangu kuwa Taasisi ya Saifee itasaidia
kupunguza rufaa za wagonjwa kwenda nje ya nchi na kupunguza gharama kwa wananchi
na Serikali kwa ujumla, hivyo uwekezaji huu una manufaa makubwa sana kwa
Taifa.”
Amesema Hospitali ya Saifee na nyingine kama hizo nchini, ni
nyenzo muhimu katika kuiharakisha Tanzania kuelekea kuwa kitovu cha utalii Tiba
katika Ukanda wa Afrika Mashariki, Kati na Kusini pamoja na Visiwa vya Bahari
ya Hindi.
Kwa upande wake, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amesema
wataendelea kuwa wabunifu na kushirikiana na sekta binafsi katika kuboresha
huduma za afya kwa Watanzania. Tanzania kuna vituo zaidi ya 12,000 vya kutolea
huduma za afya kati yake asilimia 60 ni vya Serikali na asilimia 40
vinamilikiwa na sekta binafsi.
Pia, Waziri Ummy ametumia fursa hiyo kutoa wito kwa
Watanzania wazingatie ulaji unaofaa pamoja na kufanya mazoezi ili kuepukana na
magonjwa yasiyoambukiza yakiwemo ya moyo na kisukari.
Awali, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Hospitali ya
Saifee, Murtaza Alibhai alisema hospitali yao ni taasisi ya kwanza kutoa huduma
ya upasuaji wa moyo bila kufungua kifua kwa upande wa hospitali binafsi nchini.
Alisema lengo la hospitali hiyo ni kutoa huduma bora za
matibabu kwa gharama nafuu kwa wananchi. Hospitali hiyo ina jumla ya
wafanyakazi 370 kati yao Wwatanzania ni 350 na wageni 20.
Mwenyekiti huyo wa Bodi alisema mpango wa hospitali hiyo kwa siku za hivi karibuni ni kuanza upandikizaji wa figo. Alisema hospitali hiyo mbali na kupokea wagonjwa wa ndani ya nchi, pia wamekuwa wakipokea wagonjwa kutoka nchi za Kenya, Malawi na Visiwa vya Komoro.
0 Maoni