Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mheshimiwa John Mongella amewahakikishia
wananchi wanaohama kwa hiari kutoka ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro kwenda
maeneo mengine nje ya hifadhi kuwa
serikali imejipanga na hakuna mwananchi yoyote atakayekosa haki zake iwapo
ataamua kuhama kwa hiyari.
Mheshimiwa Mongella ametoa kauli hiyo wilayani Ngorongoro
Mkoani Arusha leo tarehe 25 Januari, 2024 wakati akiwaaga wananchi 818
walioamua kuhama kwa hiyari kutoka ndani ya hifadhi hiyo na kwenda kuishi
katika Kijiji cha Msomera wilayani Handeni Mkoani Tanga.
Ameeleza kwamba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt
.Samia Suluhu Hassan ametoa fedha za kutosha ili kuhakikisha kuwa zoezi hilo
linafanikiwa na hakuna mwananchi yoyote atakayekosa kulipwa haki zake zote
zilizoanishiwa katika utekelezaji wa zoezi hilo.
Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa ameongeza kuwa zoezi hilo
linatekelezwa kwa kuzingatia misingi yote ya haki za binadamu ikiwemo kuboresha
maisha ya wananchi hao wanapofika katika Kijiji cha Msomera wilayani Handeni
Mkoani Tanga.
Kwa upande wake Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro bwana
Richard Kiiza amesema kumekuwa na muamko na ari
kubwa ya wananchi kujiandikisha na kutaka kuhama kwa hiyari ambapo katika
tukio hilo jumla ya kaya 118 zenye watu
818 na mifugo 3,129 wamehama
kwenda Kijiji cha Msomera.
Mratibu wa zoezi hilo la kuhamisha watu kutoka Hifadhi ya
Ngorongoro bwana Fedes Mdalla amesema uhamisishaji wa wananchi kuhama ndani ya
hifadhi unaendelea na zoezi hilo litakuwa linafanyika kila mara kulingana na
idadi ya nyumba zinazoendelea kujengwa na kukamilika katika eneo la mradi.
Baadhi ya wananchi walioamua kuhama kwa hiyari kwenda katika
Kijiji hicho wameishukuru serikali kutokana na jinsi inavyozingatia utu na
maslahi ya kila mmoja katika kuhakikisha kuwa wanapata stahiki zao.
Akizungumza kwa niaba ya wananchi hao Bw Sindato Ngenyike na
Bi Theresia Sabore Moko wamesema kitendo cha wao kuondoka ndani ya hifadhi kimetokana
na elimu waliyoipata kutoka kwa serikali na wananchi wenzao ambao tayari
wameshamia katika Kijiji cha Msomera.
Mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro inaendelea kuelimisha,
kuandikisha na kuhamisha wananchi kutoka ndani ya hifadhi hiyo kila wiki ikiwa
ni zoezi lenye lengo la kuboresha maisha ya wananchi na pia kulinda na
kuimarisha hifadhi.
Na mwandishi Wetu- NCAA
0 Maoni