Serikali imeeleza hatua
stahiki zilizochukuliwa kufuatia hasara iliyojitokeza kwa Serikali kupitia
Kampuni ya mafuta ya TANOIL ikiwemo hatua ya kuwasimamisha kazi wafanyakazi
wanne wa TANOIL.
Hatua hizo zimeelezwa na
Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga kwa niaba ya Naibu Waziri Mkuu na
Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko wakati akitoa ufafanuzi wa hoja
zilizowasilishwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali na Mashirika
ya Umma (CAG).
Ametaja hatua nyingine
iliyochukuliwa ni Kampuni zilizosababisha hasara hiyo kupisha TAKUKURU kufanya
kazi yake.
Amesema, Serikali inatambua
umuhimu wa Sekta ya Mafuta nchini kwa uchumi wa nchi na ndio maana imechukua
hatua kwa wote waliohusika kusababisha hasara ya takribani shilingi bilioni 7
kwa TANOIL.
"Nipende kuwataarifu
waheshimiwa Wabunge kuwa Serikali kupitia Wizara ya Nishati imeshachukua na
inaendelea na hatua za ndani kufuatia TANOIL kusababisha hasara kwa
Serikali," amesema Waziri Kapinga.
Bunge linaendelea na
majadiliano ya ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali na
Mashirika ya Umma (CAG).
0 Maoni