Miili 98 ya waliokufa kwa kufunga kuanza kupimwa

 


Vipimo vya kutumia vinasaba yaani DNA kwa miili ya watu 98 iliyokutwa kwenye msitu wa Shakahola baada ya kufunga hadi kufa, vinatarajiwa kuanza kufanyika Ijumaa ya wiki hii.

Mjumbe wa Kamati Kuu ya Afya ya Kaunti ya Kilifi, Peter Mwarogo amesema mipango inaendelea kuhakikisha mchakato huo uanaanza ili kubaini chanzo cha vifo pamoja na kuwatambua waliokufa.

Akiongea baada ya kupokea kontena maalum ya kuhifadhia maiti lililoletwa na Shirika la Msalaba Mwekundu Kenya, Mwarogo amesema watahamishia miili kwenye kontena hiyo.

Kontena hilo linauwezo wa kuhifadhi miili ya watu hadi 300, ambapo mochwari ya Malindi inauwezo wa kuhifadhi miili ya watu 30 tu, na imezidiwa kwa sasa inamiili 98.

Miili ya waumini hao waliokufa baada ya kurubuniwa na Mchungaji wao Paul Mackenzie kuwa watakutana na Yesu Kristo wakifa, itahamishwa baada ya kontena hilo kuaanza kupooza.

Kwa upande wake Mratibu wa Shirika la Msalaba Mwekundu Kenya, Hasan Musa, amesema wamerekodi idadi ya watu 322 ambao hawajulikani walipo hivyo wanapanga kuongeza nguvu kazi.

Chapisha Maoni

0 Maoni