Rais Samia azindua JNHPP, aagiza miundombinu ya usafirishaji umeme ikamilishwe

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameiagiza Wizara ya Nishati kuhakikisha miundombinu ya usafirishaji na usambazaji umeme inakamilishwa kwa haraka ili umeme unaozalishwa katika Kituo cha Kuzalisha Umeme cha Julius Nyerere (JNHPP) ufikie maeneo yenye mahitaji makubwa ya uzalishaji na uwekezaji. 

Rais Samia ametoa agizo hilo jana, Agosti 22, 2026, wakati akizindua rasmi kituo hicho kilichopo Rufiji, mkoani Pwani, akisema kukamilika kwa mradi huo kunapaswa kuleta matokeo yanayoonekana katika uzalishaji, viwanda, biashara, madini, kilimo cha kisasa, huduma za kijamii, uwekezaji na ajira. 

Kituo hicho chenye uwezo wa kuzalisha megawati 2,115, kinachangia takribani nusu ya umeme unaoingizwa katika Gridi ya Taifa, hatua ambayo imeimarisha upatikanaji wa nishati ya uhakika nchini. 

Rais Samia amesema ongezeko hilo la umeme limeondoa changamoto zilizokuwa zikiathiri shughuli za uzalishaji, uchumi na huduma nyingine muhimu, akiwataka Watanzania kutumia fursa hiyo kusukuma mbele maendeleo ya nchi. 

Amesema mradi huo umethibitisha uwezo wa Watanzania na kwamba mafanikio hayo yanapaswa kutumika kama msingi wa kutekeleza miradi mingine ya kimkakati kwa lengo la kujenga Taifa imara na linalojitegemea. 

Rais Samia pia amesema kukamilika kwa kituo hicho ni matokeo ya fikra na maono ya Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere, yaliyoendelezwa na Serikali zilizofuata katika awamu mbalimbali za uongozi. 

Katika hilo, ametambua mchango wa Marais waliomtangulia, hususan Hayati Dkt. John Pombe Magufuli, ambaye katika awamu yake alichukua hatua za kuanza utekelezaji wa ujenzi wa mradi huo mwaka 2019. 

Aidha, Rais Samia amewataka Watanzania kulinda amani na utulivu wa nchi, pamoja na kuimarisha ulinzi wa miundombinu, mazingira na vyanzo vya maji vinavyotegemewa na kituo hicho ili kiendelee kufanya kazi kwa ufanisi. 

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Kiarabu ya Misri, Dkt. Mostafa Madbouly, ameipongeza Tanzania kwa kukamilisha kituo hicho, akisema mafanikio hayo yanaonyesha uwezo wa ushirikiano wa nchi za Afrika katika kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo. 

Dkt. Madbouly amesema kukamilika kwa kituo hicho pia kumeonyesha uwezo wa kampuni za Misri katika kutekeleza miradi mikubwa kwa viwango vya kimataifa, hususan barani Afrika. 

Amesema hatua hiyo itafungua fursa zaidi za kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Misri katika maeneo ya biashara, uwekezaji, ujenzi, barabara, bandari, kilimo, umeme na nishati. 

Naye Waziri wa Nishati, Deo Ndejembi, amesema Serikali inaendelea kujenga njia ya kusafirisha umeme ya kilovolti 400 ya Iringa–Mbeya–Songwe–Rukwa, ambayo imefikia asilimia 98 ya utekelezaji. 

Amesema Serikali pia inaendelea na ujenzi wa njia za Songea–Tunduru–Masasi–Maumbika na Tanzania–Uganda, zitakazosaidia kuunganisha vituo vya uzalishaji umeme, maeneo ya shughuli za kiuchumi na masoko ya kikanda. 

Ndejembi amesema Tanzania imeanza mazungumzo ya kuuza umeme nchini Zambia, huku ikiwa na makubaliano ya kubadilishana umeme na Kenya na ikiendelea na majadiliano na nchi nyingine jirani. 

Akitoa salamu zake, Rais Mstaafu wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Dkt. Akinwumi Adesina, amesema kituo hicho kimeiweka Tanzania katika nafasi nzuri ya kuwa kitovu cha uzalishaji nishati na shughuli za kiuchumi katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati. 

Dkt. Adesina amesema upatikanaji wa nishati ya uhakika utawezesha Tanzania kuongeza thamani ya rasilimali, kukuza biashara na kutengeneza ajira zaidi. 

Ujenzi wa Kituo cha Kuzalisha Umeme cha Julius Nyerere ulianza mwaka 2019 kwa gharama ya Sh7.452 trilioni. Kituo hicho kina mitambo tisa yenye uwezo wa kuzalisha jumla ya megawati 2,115, jengo la mitambo, transfoma 27 na kituo cha kupokea na kusafirisha umeme kwa msongo wa kilovolti 400.




Chapisha Maoni

0 Maoni