Na. Beatus Maganja - TAWA
Miaka 10 iliyopita Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania - TAWA ilianza safari ikiwa imekabidhiwa jukumu kubwa la kusimamia na kuhifadhi sehemu muhimu ya rasilimali ya wanyamapori wa Tanzania. Leo, katika mwaka wake wa 10 tangu kuanza kazi rasmi mwaka 2016, Hifadhi ya Selous imetwaa tuzo ya Kivutio Bora cha Utalii Barani Afrika 2026, huku Hifadhi ya Mpanga-Kipengere ikishinda tuzo ya Eneo Bora la Fungate Barani Afrika 2026 katika Tuzo za Utalii Duniani (World Travel Awards–WTA).
Kwetu, vikombe hivi havisemi tu kwamba tumeshinda, bali vinazua swali kubwa zaidi: kama haya yamewezekana katika miaka 10 ya kwanza, Je miaka 10 ijayo inaweza kuibua nini?
Ushindi wa Mpanga-Kipengere unatupa somo kubwa. Hiki ni kivutio ambacho hakijapata mwonekano mkubwa katika masoko mapana ya kimataifa kama baadhi ya maeneo ya utalii yaliyojijengea majina kwa muda mrefu, lakini kimeweza kushinda katika ushindani uliokuwa na majina makubwa ya Afrika. Hilo linatufanya TAWA tujiulize: je, thamani ya baadhi ya maeneo tunayoyasimamia ni kubwa zaidi kuliko kiwango ambacho tumefanikiwa kuiambia dunia mpaka sasa?
Ndiyo maana baada ya ushindi huu hatujiulizi tu, “tutashinda tuzo gani nyingine?” Tunajiuliza, “ni eneo gani jingine tunalosimamia ambalo dunia bado haijaliona kwa ukubwa wake?”
Ndani ya maeneo ya TAWA kuna wanyamapori, mito, maziwa, maporomoko ya maji, milima, mabonde na maeneo makubwa ya asili ambayo hayajaingiliwa sana na shughuli za binadamu, yenye uwezo wa kutoa aina mbalimbali za utalii. Mpanga-Kipengere imetufundisha kwamba wakati mwingine changamoto si kukosa kivutio bora, bali kukipa jukwaa linalolingana na thamani yake.
Kwa Kaimu Kamishna wa Uhifadhi wa TAWA, Mlage Y. Kabange, kupokea vikombe hivyo Zanzibar kulikuwa zaidi ya kupokea tuzo kwa niaba ya Mamlaka. Utambuzi huo wa kimataifa unaongeza wajibu wa kuhakikisha mwonekano unaopatikana leo unatafsiriwa kuwa fursa za masoko, huduma bora, miundombinu, uwekezaji na hatimaye wageni wengi zaidi. Tuzo inakuwa na maana kubwa zaidi inapohama kutoka jukwaani na kuingia kwenye uchumi.
Ndiyo maana pia kauli ya Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TAWA, Meja Jenerali (Mstaafu) Hamis R. Semfuko, kwamba Watanzania wajiandae na “kishindo” kingine mwaka ujao ina maana pana. Kishindo hicho. si lazima kiwe kombe jingine pekee bali kinaweza kuwa kivutio kingine kuibuliwa, uwekezaji mpya kuingia au eneo ambalo leo halipo katika ratiba za safari za watalii wengi kuanza kutafutwa katika masoko ya kimataifa.
Katika safari hii, TAWA haiko peke yake. Chini ya mwelekeo wa kisera wa Wizara ya Maliasili na Utalii, mafanikio haya yana nafasi ya kuongeza nguvu ya Tanzania kama eneo kuu la utalii. Kadiri vivutio vingi zaidi vinavyotambulika, ndivyo Tanzania inavyoongeza sababu za mtalii kuja, kutembelea maeneo mengi zaidi, kukaa muda mrefu na kuongeza mchango wa utalii katika uchumi.
Kwa hiyo, tunapotazama vikombe hivi katika mwaka wetu wa 10, hatuvioni kama alama ya kufika; bali tunaviona kama ishara ya kile ambacho bado hakijagunduliwa. Selous na Mpanga-Kipengere zimefungua pazia, lakini nyuma yake kuna hazina nyingine nyingi zinazosubiri nafasi yake. Miaka 10 ya kwanza imetufikisha kwenye jukwaa la Afrika; sasa tunaanza muongo mwingine tukiwa na swali jipya kwamba dunia ikiwa imeanza kuona tulichonacho, je, iko tayari kuona kilichobaki?

0 Maoni