WAZIRI
wa Madini, Anthony Mavunde, amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini
ya Rais Samia Suluhu Hassan itaendelea kuboresha mazingira ya
uwekezaji ili kuvutia na kuwezesha miradi zaidi ya madini
nchini.
Mavunde ameyasema hayo baada ya kufanya mazungumzo na
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Marvel Gold ya Australia, Timothy
Strong, ambaye alifika kutoa taarifa ya maendeleo ya mradi wa
uchimbaji wa dhahabu unaotarajiwa kuanzishwa katika Wilaya ya Hanang,
Mkoa wa Manyara.
Amesema Serikali imefurahishwa na kasi ya
utekelezaji wa hatua za awali za mradi huo, ambao kwa sasa upo katika
hatua ya uchorongaji baada ya kukamilisha utafiti wa awali kwa
kutumia teknolojia ya ndege zisizo na rubani (drones).
“Tunapongeza
wawekezaji kwa kasi wanayoionesha katika kuendeleza mradi huu muhimu.
Serikali itaendelea kushirikiana nao kuhakikisha sekta ya madini
inachangia kikamilifu katika uchumi wa taifa,” amesema
Mavunde.
Kwa upande wake, Strong amesema kampuni hiyo
imeipongeza Serikali ya Tanzania kwa mazingira rafiki ya uwekezaji,
akibainisha kuwa hatua ya awali ya uchorongaji inatarajiwa kukamilika
mwishoni mwa Julai 2026.
Amesema lengo la kampuni ni kuanza
uzalishaji wa madini mara baada ya kukamilika kwa taratibu zote za
kiufundi na kisheria.
Mradi huo unatarajiwa kutoa ajira na
kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika Wilaya ya Hanang na
Mkoa wa Manyara kwa ujumla.

.jpeg)
0 Maoni