Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) imeandika historia nyingine baada ya jopo la madaktari bingwa na wataalamu wa afya kufanikisha salama uzazi wa watoto watano kwa wakati mmoja kwa Bi. Victoria Mkwizu, mkazi wa Tabata jijini Dar es Salaam.
Watoto
hao wamezaliwa tarehe 13 Juni 2026 na wanaendelea vizuri chini ya
uangalizi wa wataalamu wa hospitali hiyo, ambapo watatu ni wa kiume
na wawili ni wa kike.
Akiwa wodini, Bi. Victoria amesema
anafurahia huduma alizopata katika Hospitali ya Taifa Muhimbili tangu
alipopokelewa hadi kujifungua salama watoto hao watano.
Amewapongeza
madaktari, wauguzi na wataalamu wengine wa afya kwa uangalizi wa
karibu waliompatia katika kipindi chote cha matibabu, akieleza kuwa
mchango wao umewezesha yeye na watoto wake kuendelea vizuri.
Kwa
niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili,
Mkurugenzi wa Huduma za Upasuaji, Dkt. Rachel Mhaville amesema tukio
hilo ni la kipekee na limehitaji ufuatiliaji wa karibu kutoka kwa
timu ya wataalamu wa hospitali hiyo ili kuhakikisha usalama wa mama
na watoto huku akimpongeza Bi. Victoria kwa kujifungua salama watoto
hao watano na kuwatakia afya njema.
Aidha Dkt. Mhaville
amesema Muhimbili itagharamia gharama zote za matibabu za Bi.
Victoria na watoto wake kuanzia alipolazwa hospitalini tarehe 15 Mei
2026 hadi watakapomaliza matibabu na kuruhusiwa kurejea nyumbani.
Amesema hatua hiyo ni sehemu ya jitihada za hospitali kuhakikisha mama na watoto wanaendelea kupata huduma bora na salama katika kipindi hiki muhimu.


.jpeg)
0 Maoni