Na. Beda Msimbe,TBN, Moscow
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan
ambaye yupo hapa Shirikisho la Urusi kwa ziara ya kitaifa anatarajiwa
kutunukiwa Shahada ya Uzamivu na Chuo Kikuu cha RUDN nchini
hapa.
Tuzo hiyo inatokana na kutambua kazi yake na mchango
wake katika jamii ya Tanzania na dunia katika masuala ya msingi
yanayohusu maisha ya binadamu.
Chuo cha RUDN chenye wanafunzi
wa Kitanzania 570 kufikia mwaka 2025, katika miaka zaidi ya 65 ya
RUDN, Watanzania 1,132 wamepitia chuo hicho.
RUDN kimesomesha
zaidi ya wataalamu 200,000 duniani na sasa kina watu 44,000 kutoka
nchi 160 duniani. Chuo hiki ni cha 367 kwa ubora duniani kwa mujibu
wa QS World University Ranking ya mwaka 2025.
Rais Dkt. Samia
ambaye amepokelewa jana na Waziri wa Maendeleo ya Uchumi wa Urusi
Maxim Reshetnikov anatarajiwa kukutana na mwenyeji wake Rais Vladimir
Putin na kufanya mazungumzo ya ana kwa ana kwa ajili ya kuimarisha
uhusiano wa kidiplomasia na kiuchumi.
Aidha, akiwa nchini
hapa, akiwa kiongozi wa pili wa Tanzania kutembelea Urusi, ziara ya
kwanza ikiwa imefanywa na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere,
atashiriki Jukwaa la Uchumi la St. Petersburg ambapo Tanzania itanadi
fursa za uwekezaji na diplomasia ya uchumi kwa viongozi, wawekezaji
na watunga sera wa kimataifa.
Katika kufanikisha Dira ya Taifa
ya Maendeleo 2050, ziara hii ni kichocheo cha utekelezaji kwa
mafanikio ya dira hiyo ambayo inahitaji rasilimali watu wenye
utaalamu na upeo mkubwa kusimamia na kuendesha miradi ya kimkakati
itakayopelekea ajira, viwanda na biashara zitakazoingiza dola
trilioni moja na kuwa katika uchumi wa kati wa juu.
Katika
WhatsApp yake, Rais Samia amesema ziara hiyo ni muhimu hasa taifa
linapoelekea kuanza utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050
ambayo inataka ushiriki mkubwa wa sekta binafsi.
"Tutafanya
mazungumzo na wenyeji wetu yanayolenga kuimarisha ushirikiano katika
sekta za kimkakati zinazogusa maisha ya wananchi."
"Aidha,
tutashiriki majukwaa ya biashara na uwekezaji na kutangaza fursa
zilizopo nchini, pamoja na kufungua zaidi fursa za masoko kwa bidhaa
za Tanzania nchini Urusi."

0 Maoni