Rais Dk. Mwinyi Asisitiza Maslahi ya Taifa Mazungumzo ya SUK Zanzibar

 

Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar na Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Mwinyi amesema kuwa mazungumzo ya kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) kati ya CCM na ACT-Wazalendo yanaendelea vizuri huku chama chake kikiweka mbele maslahi ya taifa, serikali, na chama hicho kwa ujumla.

Akizungumza jana na viongozi pamoja na wanachama wa CCM Mkoa wa Kaskazini Unguja katika mkutano wa shukrani baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025 uliofanyika katika ukumbi wa Ofisi za CCM Mahonda, Dk. Mwinyi alibainisha kuwa CCM inaheshimu mfumo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa uliowekwa kikatiba na kisheria lakini akasisitiza kuwa hawatakubali kuburuzwa katika mchakato huo unaoendelea.

Alifafanua kuwa serikali itaendelea kutekeleza majukumu yake kama kawaida hata kama ACT-Wazalendo hawatayawasilisha majina ya viongozi wao kwa ajili ya nafasi za Makamu wa Kwanza wa Rais na mawaziri wanne kama sheria inavyoelekeza, kwani hadi sasa chama hicho kimeshindwa kufanya hivyo kwa kile walichodai kuwa na malalamiko na mapendekezo yao.

Dk. Mwinyi alieleza kuwa ushindi wa CCM katika uchaguzi mkuu uliopita umeonesha ukomavu mkubwa wa kisiasa na kuifanya Zanzibar kuandika historia ya kipekee ya kufanya uchaguzi wa amani na utulivu.

Aliwataka wanachama kuanza kufanya tathmini ya kina ya uchaguzi huo na kuanza kujiandaa mapema kwa ajili ya uchaguzi wa ndani wa chama uliopangwa kufanyika mwaka 2027 na hatimaye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2030. Rais alisisitiza umuhimu wa kudumisha umoja ndani ya chama kwa kuondoa makundi yasiyo na tija, kuimarisha mfumo wa ulipaji ada, na kuendeleza mafunzo ya itikadi kwa wanachama wote ili kukiongezea chama uimara.

Aidha, alionya dhidi ya baadhi ya viongozi ambao wamekuwa wakianzisha makundi kwa ajili ya maslahi yao binafsi akisema jambo hilo ni hatari kwa ustawi wa CCM. Alimalizia kwa kutoa wito kwa viongozi kuwa wabunifu zaidi katika kuimarisha uchumi wa chama kupitia uwekezaji makini wa rasilimali zilizopo zikiwemo viwanja na majengo ili kuongeza mapato na kukiwezesha chama kujiendesha kwa ufanisi zaidi.

#MezaYaUmoja

Chapisha Maoni

0 Maoni