Mawakili
wa Serikali wamehimizwa na kusisitizwa kuendelea kusimamia mashauri
ya Serikali na kuitetea Serikali kwa ujumla katika vyombo vya ndani
na nje ya nchi.
Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Katiba na
Sheria, Mhe. Zainab Katimba (Mb), wakati akifunga mafunzo kwa
Mawakili wa Serikali wa kutoka Wizara mbalimbali, taasisi za
Serikali, Mamlaka za Mikoa na Serikali za Mitaa wa Tanzania Bara na
Zanzibar. Mafunzo hayo yameandaliwa na Ofisi ya Wakili Mkuu wa
Serikali ambayo yamefanyika kwa muda wa siku tatu kuanzia tarehe 18
hadi 22 Mei, 2026 jijini Arusha.
Mhe. Katimba amesema kuwa
Serikali inawategemea sana Mawakili wa Serikali katika kulinda
rasilimali za Taifa kupitia ushauri wa kisheria wenye tija na
usimamizi madhubuti wa mashauri mbalimbali.
“Hivyo, baada ya
mafunzo haya tunatarajia muweze kusimamia kwa ufanisi mashauri ya
Serikali; kuimarisha usimamizi wa mikataba na manunuzi ya umma;
kushauri vizuri Serikali kuhusu sheria za kodi, anga na uwekezaji;
kusimamia kwa weledi usuluhishi wa migogoro; na kuitetea Serikali kwa
ufanisi katika vyombo vya ndani na kimataifa,” amesema Mhe.
Katimba.
Pia, ameongeza kuwa mafunzo hayo yamekuja wakati
muhimu ambapo Taifa linaelekea katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya
Maendeleo 2050 inayolenga kujenga uchumi wa kati unaojumuisha
wananchi wote. Ili kufikia malengo hayo, ni muhimu kuwa na taasisi
imara za kisheria pamoja na wataalamu wenye uwezo wa kusimamia
sheria, mikataba, uwekezaji, kodi na utatuzi wa migogoro kwa haki,
uwazi na uwajibikaji.
“Kupitia ujuzi mlioupata, nina imani
kuwa mtakuwa sehemu muhimu katika kuhakikisha kuwa sheria na mifumo
ya Serikali inasimamiwa kwa weledi na kwamba matunda ya maendeleo
yanawanufaisha wananchi wote kupitia mazingira bora ya uwekezaji,
biashara na utoaji wa huduma za umma,” amesisitiza Mhe.
Katimba.
Wakili Mkuu wa Serikali, Dkt. Ally Possi amemueleza
Mhe. Katimba kuwa, Mawakili hao wamepatiwa mafunzo na wakufunzi
wabobezi wa taaluma mbalimbali ambapo mada mbalimbali zimetolewa
zinazohusu dhamana za kibenki, usuluhishi wa ndani na nje ya nchi,
usimamizi wa mikataba, sheria za kodi, sheria za anga pamoja na namna
ya kuitetea Serikali katika mabaraza ya kimataifa ya
uwekezaji.
“Mada hizi ni muhimu sana katika kuhakikisha
Serikali inalindwa dhidi ya hasara na migogoro inayoweza kuzuilika
kwa kuwa Mawakili wa Serikali sio tu Mawakili ila ni walinzi wa
kalamu wanaolinda uchumi na rasilimali za taifa,” amesema Dkt. Ally
Possi.
Pia, Dkt. Possi ameongeza kuwa Mawakili wa Serikali
watazingatia mabadiliko ya nchi yetu yanayotarajiwa kutokea katika
utekelezaji wa Dira ya Maendeleo 2050 na mwenendo wa dunia katika
masuala mbali mbali.
Mafunzo haya yamefanyika kwa mara ya saba
mfululizo ambapo yamekuwa yanafanyika mara moja kwa mwaka na
yanaratibiwa na kuandaliwa na Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali.



0 Maoni