Waziri Mkuu Mstaafu Mizengo Pinda atoa ujumbe mzito wa
Mwaka Mpya akiitaka jamii kulinda uzalendo huku Serikali mkoani Katavi ikitaja
mapinduzi ya miundombinu kama jibu la maendeleo kwa wananchi.
Waziri Mkuu huyo Mstaafu wa Awamu ya Nne akilaanii
machafuko hayo yaliyotokea Oktoba 29,2025 alisema wazi kuwa yale hayakuwa
maandamano ya amani kama yalivyodhaniwa na wengi.
Akizungumza kwa uchungu na msisitizo wa kizalendo wakati wa
sherehe za Mwaka Mpya zilizofanyika katika Shule ya Sekondari ya Mizengo Pinda
iliyopo Kibaoni mkoani Katavi, mzee Pinda amefafanua kuwa kundi la vijana
lilishiriki mipango ya makusudi ya kuharibu mali za watu, miundombinu ya umma
na kutaka kuvuruga amani ya nchi ambayo ndiyo hazina kuu ya Watanzania.
Waziri Mkuu huyo mstaafu ameweka wazi kuwa vitendo hivyo ni
kinyume na ustaarabu wa taifa hili na ameitaka jamii kurejea katika misingi ya
malezi bora ili kujenga vijana waadilifu na wazalendo ambao hawawezi kutumiwa
kama nyenzo ya kuligawanya taifa au kubomoa kile kilichojengwa kwa jasho na
damu.
Katika hafla hiyo iliyohudhuriwa na ndugu jamaa marafiki
pamoja na viongozi wa taasisi mbalimbali za serikali mzee Pinda ametumia fursa
hiyo kutoa onyo kwa wazazi na walezi akisisitiza kuwa jukumu la kuliokoa taifa
dhidi ya machafuko ya baadaye linaanzia kwenye ngazi ya familia.
Amesema kuwa vijana waliostaarabika hawawezi kushawishika
kijinga kujiingiza kwenye vitendo vya kihalifu vinavyovika koti la maandamano
ya amani na hivyo malezi ya kimaadili ni silaha pekee ya kulinda usalama wa
nchi yetu kwa miaka ijayo.
Ujumbe huo wa mzee Pinda umepokelewa na wageni waalikwa
kama sauti ya busara inayolenga kuliponya na kuliunganisha taifa kufuatia
makovu ya machafuko ya Oktoba 29,2025 huku kukiwa na msisitizo wa kudumisha
umoja na utulivu uliopo.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Mlele Abdulmajid Mwanga
akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Katavi ameelezea juhudi za serikali katika kuibua
fursa za kiuchumi kama njia ya kuwapunguzia wananchi kero na kuwafanya wawe na
matumaini ya maendeleo badala ya kujiingiza kwenye vurugu.
Mkuu huyo wa wilaya amebainisha kuwa serikali inaendelea na
utekelezaji wa miradi mikubwa ikiwemo ujenzi wa barabara ya Sitalike hadi
Kibaoni kwa kiwango cha lami mradi ambao ulikuwa umekwama kwa miaka mingi na
kusababisha adha kubwa kwa wasafiri na wafanyabiashara. Kukamilika kwa
miundombinu hiyo ya barabara ni sehemu ya mikakati ya serikali ya awamu ya sita
ya kufungua mkoa wa Katavi na kuhakikisha kuwa huduma za usafirishaji wa abiria
na mizigo zinaimarika ili kuchochea ukuaji wa uchumi wa mtu mmoja mmoja na
taifa kwa ujumla.
Ujumbe uliotolewa katika hafla hiyo ya Mwaka Mpya nyumbani
kwa mzee Pinda umetafsiriwa kama dira muhimu kwa Watanzania wote katika kuanza
mwaka mpya kwa kutafakari thamani ya amani na madhara ya machafuko.
Baadhi ya washiriki wa hafla hiyo wamesema kuwa maneno ya
kiongozi huyo mstaafu yamejikita katika kurejesha mshikamano wa kitaifa na
kuwakumbusha vijana kuwa maendeleo ya kweli hayaji kwa njia ya fujo bali kwa
njia ya kufanya kazi na kulinda miundombinu inayojengwa na serikali.
Hakika sauti ya mzee Pinda imesikika kama mbiu ya mgambo
inayotaka kila mwananchi kuwa mlinzi wa amani ya mwenzake huku ikilaani kila
aina ya jaribio la kutaka kurudisha nyuma hatua za kimaendeleo ambazo Tanzania
imepiga hadi sasa.

0 Maoni