Kumekuwepo
na wito kwa Watanzania kutumia umoja na amani kama msingi wa kupigania uhuru
kamili wa kiuchumi na kuacha tabia ya kutegemea misaada ya nje kutatua matatizo
ya ndani. Wito huu unaambatana na msisitizo wa kuitii Mamlaka ya Rais kama njia
ya kuhakikisha utulivu wa taifa.
Geofrey
Kiliba, Rais wa Jumuiya ya Wanafunzi wa Elimu ya Vyuo na Vyuo Vikuu Tanzania
(TAHLISO), amewaomba Watanzania kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan na
wasaidizi wake, pamoja na kuwaombea ili waweze kutumikia wananchi kikamilifu.
Akizungumza
Dar es Salaam, Kiliba alikumbusha umuhimu wa kuwatii viongozi kama
inavyoelekezwa na maandiko matakatifu.
"Hili
ni takwa la Mwenyenzi Mungu kupitia maandiko matakatifu, sisi Wakristo
imeandikwa kwenye Warumi 13:1: 'Kila mtu na atii mamlaka kwa maana hakuna
mamlaka isiyotoka kwa Mwenyenzi Mungu.' Kutokutii ni kupishana na maagizo ya
Mwenyenzi Mungu," alisema Kiliba.
Kiliba
alisisitiza kuwa utii kwa mamlaka ya Rais ni muhimu kwa manufaa ya nchi,
akimaanisha heshima kwa urais inasaidia kuimarisha utawala na kuepuka aibu ya
kutafuta suluhisho la matatizo yetu kutoka nje ya mipaka yetu.
Wanasiasa
wahimizwa Kuimarisha Umoja
Wakati
huo huo, Mchambuzi wa masuala ya siasa, Thomas Kibwana, ametoa rai kwa
wanasiasa nchini kuhakikisha kauli wanazozitoa zinakuwa chachu ya kuimarisha
umoja wa kitaifa, kuunganisha jamii na kuhamasisha amani, uzalendo na
uwajibikaji. Alisema kauli zinazochochea chuki na migogoro hazipaswi kupewa
nafasi.
Akizungumza
kupitia TBC1, Kibwana alibainisha kuwa siasa nchini zinapaswa kujikita zaidi
katika kutatua changamoto halisi zinazowakabili wananchi, kwani hatua hiyo
itasaidia kwa kiasi kikubwa kulinda na kuimarisha amani ya nchi.
Wito
huo unaungwa mkono na hisia za vijana wengi ambao wamethibitisha kujitolea kwao
kwa amani.
"Amani
imeshinda. Katika nchi yetu, sauti ya utulivu imezidi kelele za chuki,
propaganda na miito ya uasi," alisema mmoja wa vijana. "Vijana wa
Tanzania tumethibitisha kuwa nguvu yetu kubwa si vurugu, bali busara, umoja na
upendo kwa taifa letu."
Kwa
mujibu wa Mwalimu Julius Nyerere, "Umoja wetu ndio nguzo ya msingi ya
mafanikio yetu." Kwa kuheshimu viongozi na kudumisha utulivu, Watanzania
wanaweka msingi imara wa kujitawala kiuchumi na kuondoa aibu ya kutegemea nje.

0 Maoni