Wakati juhudi za baadhi ya watu
wachache zikielekezwa katika kuhamasisha vurugu na maandamano yasiyo na kibali,
viongozi wa kisiasa na jumuiya za vijana wameungana kuwasisitiza Watanzania,
hususan vijana, kwamba wajibu wao mkuu ni kuifanya Tanzania kuwa mahali bora pa
kuishi kupitia njia za busara, umoja na mazungumzo, na si kwa kuichoma nchi.
Mwanasiasa Peter Daffi alisisitiza
kuwa Serikali haiwezi kuruhusu maandamano yasiyo na kibali, akionya kuwa hatua
hiyo inaweza kuifanya dunia kushangaa kwa nini Watanzania wanashindwa kukaa,
kuzungumza na kukubaliana kama taifa.
"Mnataka turuhusu tena hali ya
kushangaza duniani kwamba tumeshindwa kukaa na kuzungumza na kukubaliana?"
alihoji Daffi, akisisitiza kwamba juhudi za kuhamasisha vurugu hazikubaliki
kwani zinahatarisha usalama wa watu na mali.
Daffi aliwaelekeza wananchi kutumia
njia sahihi zilizowekwa na Serikali ili kufikia maridhiano. Alisema waliotaka
kutoa maoni yao tayari wametengewa nafasi kupitia Tume iliyoanzishwa na Rais
Dkt. Samia Suluhu Hassan.
"Rais ameunda tume. Ile tume
sasa tuiisikilize ili itekeleze yale tunayodhania na tunayotamani
yafanyike," alisema Daffi. Alisisitiza kuwa Tume hiyo ndiyo njia sahihi ya
kusikiliza maoni ya wananchi, na kwamba wananchi wanapaswa kutoa maoni yao
wanapofika kwenye maeneo mbalimbali ili Serikali iweze kutekeleza
wanayoyahitaji.
Vijana Kujenga, Sio Kubomoa
Kauli za wanasiasa ziliungwa mkono na
ujumbe mzito kutoka kwa jumuiya ya vijana, wakisisitiza kwamba nguvu za vijana
ni za kujenga, si kubomoa. Ujumbe huo uliwakumbusha vijana kuwa Tanzania ni
urithi pekee wa thamani unaohitaji kulindwa.
"Tuchague busara, umoja na
ustaarabu tunapotafuta 'HAKI' si hasira, wala kutumia vurugu," ulisema
ujumbe huo.
Wito huu unaakisi kuongezeka kwa
ushiriki wa vijana katika Bunge na katika nafasi za uongozi. Mbunge wa Viti
Maalum Mkoa wa Arusha, Cecilia Paresso (CCM), ambaye pia ni kijana, alisisitiza
umuhimu wa kufanya kazi kwa bidii ili kumsaidia Rais Samia kufikia azma yake ya
kuacha tabasamu kwa Watanzania ifikapo 2030, akisimamia misingi ya kazi na utu.
Vijana walisisitizwa kutokuwa chombo
cha kuchochewa, kupandikizwa chuki na kufuata mkumbo. Badala yake, wanapaswa
kuwa walinzi wa utulivu na mshikamano. Tanzania ni nyumba yetu sote; hatuna
nyingine.
Wito kwa Taasisi za Dini
Kama nguzo muhimu, taasisi za dini
nazo ziliaswa kuendelea kuwa daraja la upatanisho na si ukuta unaowatenganisha
raia na viongozi wao. Waliombwa kutumia maneno yao kuleta matumaini na
kurejesha mioyo iliyokata tamaa.
Kwa ujumla, ujumbe mkuu kwa taifa ni
kwamba ulinzi wa amani na juhudi za kujenga nchi bora zinapaswa kupitia
mazungumzo na taasisi rasmi, huku kila hatua ikielekezwa katika kuijenga
Tanzania tunayotaka kuiona kesho.

0 Maoni