Makamu wa
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi
amesema Serikali inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imechukua hatua
za kurejesha utengamano katika nchi na kuhakikisha wananchi wanaishi katika
utawala wa sheria.
Makamu wa
Rais amesema hayo wakati akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Mkutano wa Dharura wa Wakuu wa Nchi na
Serikali wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini Mwa Afrika (SADC),
uliyofanyika kwa njia ya mtandao, akiwa mkoani Dodoma.
Amesema
dhamira ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha mchakato wa mazungumzo
ya maridhiano unafanikiwa ili kuwa na Taifa lenye amani na umoja na kuendelea
kuwa mfano wa utulivu katika Afrika na Dunia kwa ujumla.
Halikadhalika,
Makamu wa Rais amesema Tanzania ni salama na tulivu na ipo tayari kuendelea
kupokea wageni kutoka duniani kote kwa manufaa ya nchi zote.
Aidha,
Makamu wa Rais, amewashukuru viongozi wa SADC walioshiriki uapisho wa Rais Dkt.
Samia Suluhu Hassan pamoja na wote waliotoa pongezi za dhati. Amesema jitihada
zote zitatumika kuhakikisha Tanzania inapata maendeleo na amani kuendelezwa.
Mkutano huo
umempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu
Hassan kwa ushindi aliyoupata na uchaguzi wenye mafanikio.
Mkutano huo
ulilenga kujadili kujiondoa kwa nchi ya Madagascar kama nchi Mwenyekiti wa
SADC, ambapo nchi ya Afrika Kusini imependekezwa kuwa Mwenyekiti kwa kipindi
cha mpito mpaka kufikia mwezi Agosti 2026.
Mkutano huo
umekubaliana kuendelea kutumia kauli mbiu ya Mkutano wa 45 wa SADC uliyofanyika
nchini Madagascar ambayo ni “Kuimarisha Viwanda, Mapinduzi ya Kilimo,
Mabadiliko ya Nishati kwa SADC yenye Uhimilivu”


0 Maoni