Kuelekea uchaguzi Mkuu,
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limejipanga vizuri kuhakikisha Amani, Utulivu na
Usalama vinatawala muda wote.
Akizungumza mara baada
ya kufanya doria za Magari, Miguu na Mbwa wa Polisi kuzunguka maeneo mbalimbali
ya Jiji la Mbeya, Kamanda wa Polisi Mkoani humo Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa
Polisi (SACP) Benjamin Kuzaga amewataka wananchi kujitokeza siku ya jumatano
Oktoba 29, 2025 kupiga kura.
"Tangu kuanza kwa
kampeni hadi sasa hali ya usalama Mkoa wa Mbeya ni shwari, hakuna matukio wala
viashiria vya uvunjifu wa amani, Jeshi la Polisi lipo imara na limejipanga
vizuri kuhakikisha usalama wa raia na mali zao unaendelea kuimarishwa"
alisema Kamanda Kuzaga.
Aidha, Kamanda Kuzaga amesisitiza
wananchi kupuuza maneno ya uongo, upotoshaji, taarifa zisizo sahihi
zinazotolewa kupitia mitandao ya kijamii kuhamasisha vurugu na vitendo vya
uvunjifu wa amani na kuwahakikishia Wananchi usalama.
Sambamba na hilo,
Kamanda Kuzaga amesema Jeshi hilo halitasita kuchukua hatua kali kwa mujibu wa
sheria kwa yeyote atakayejaribu kuvuruga Amani, Utulivu na Usalama kuelekea
uchaguzi Mkuu.


0 Maoni