Wakandarasi wote waliopewa zabuni ya kutekeleza miradi
mbalimbali ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA, wametakiwa kuhakikisha miradi
hiyo inakamilika kwa wakati na kwa ubora uliopangwa ili iweze kuwanufaisha
wananchi.
Rai hiyo imetolewa Agosti 31, 2025 wilayani Korogwe na
Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Mhe. Balozi Meja Jenerali Mstaafu
Jacob Kingu, wakati akizungumza na
Wakandarasi wa miradi ya umeme wanaotekeleza miradi hiyo mkoani Tanga.
"Katika utekelezaji wa miradi hii bado kuna changamoto
ya uunganishaji mdogo wa wateja kwa sababu mbalimbali na kufanya miradi hii
kutokumalizika kwa wakati, hakikisheni mnaongeza kasi, maarifa ya kuwahudumia
wateja na ubunifu ili uunganishaji uweze kuleta tija," amesisitiza Mhe.
Balozi Kingu.
Katika hatua nyingine, Balozi Kingu amesema mkoa wa Tanga
vijiji vyote 763 vimeshapata huduma ya umeme kupitia miradi ya REA na vitongoji
2,382 kati ya vitongoji 4,531 navyo vimepata huduma ya umeme na kasi kubwa
inaendelea ya kuwaungashia wateja katika maeneo yao.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati
Vijijini (REA), Mha. Hassan Saidy amemtaka mkandarasi Ok electrical and
Electronics Services Ltd na Wakandarasi
wengine kuhakikisha wanaongeza kasi ya kupeleka umeme kwa wateja ili wateja
wengi wapate huduma hiyo.
"Sisi REA tutaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya
umeme pamoja na kuwasimamia kwa karibu wakandarasi wote waliopewa zabuni ya
kutekeleza miradi hii ili iweze kuwa na mchango mkubwa kwa jamii," amesema
Mha. Saidy.
Naye, Kaimu Mhandisi Miradi ya REA Mkoa wa Tanga, Mha.
Kelvin Melchiad amesema, Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA)
imetoa jumla ya kiasi cha shilingi bilioni 68.5 ili kuhakikisha miradi yote
inatekelezwa na wananchi wanapatiwa huduma ya umeme ili kuwapatia maendeleo ya
kiuchumi na kijamii.
Wakandarasi waliohudhuria kikao hicho ni mkandarasi Ok electrical and Electronics Services Ltd, Tontan Project Technology Co. Ltd na Transpower Ltd and Whitecity International Contractor Ltd.
0 Maoni