Tume Huru ya Uchaguzi (INEC) imetoa mwaliko kwa vyombo vya habari vyenye nia ya kuripoti shughuli za kupiga kura, kuhesabu kura na kutangaza matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, kuwasilisha maombi ya kupata vibali rasmi.
Kupitia
taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Uchaguzi, Kailima Ramadhani Kailima, tume
hiyo imeeleza kuwa vyombo vyote vya habari vinavyotaka kushiriki katika
kuripoti uchaguzi huo, vinapaswa kuwa na sifa mbili kuu kabla ya kuwasilisha
maombi.
“Chombo cha
habari kinapaswa kiwe kimesajiliwa kwa mujibu wa Sheria ya Huduma za Vyombo vya
Habari ya mwaka 2016, na pia kuhakikisha waandishi wake wamethibitishwa na Bodi
ya Ithibati ya Waandishi wa Habari, wakiwa na Press Cards halali zilizotolewa
na bodi hiyo,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.
INEC
imefafanua kuwa maombi ya vibali hivyo yatawasilishwa kwa njia ya mtandao
kupitia Mfumo wa Usajili wa Kibali ujulikanao kama Accreditation Management
System (AMSA) unaopatikana kupitia kiungo: https://ams.inec.go.tz.
Dirisha la
kupokea maombi litaanza rasmi Septemba 3, 2025 na kufungwa Oktoba 3, 2025.
Aidha,
Mkurugenzi wa Uchaguzi Kailima amesisitiza kuwa Tume haitatoa rasilimali yoyote,
iwe fedha au aina nyingine kwa vyombo vya habari vitakavyopata kibali, na
kwamba vyombo hivyo vinapaswa kujitegemea kwa uendeshaji wa shughuli zao wakati
wa uchaguzi.
Hatua hii
inalenga kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa uwazi, huku vyombo vya habari
vikichangia kwa weledi katika kutoa taarifa sahihi kwa umma kuhusiana na
mchakato mzima wa uchaguzi.
0 Maoni