CRDB kufunga huduma kwa siku tatu ili kuboresha teknolojia

 

Benki ya CRDB imetangaza kuwa itafunga huduma zake zote kwa muda wa siku tatu mfululizo, kuanzia Ijumaa ya Septemba 5 hadi Jumapili ya Septemba 7, 2025, ili kutoa nafasi kwa maboresho ya mifumo ya kiteknolojia.

Taarifa rasmi iliyotolewa leo kwenye akuanti ya CRDB na uongozi wa benki hiyo, imeeleza kuwa hatua hiyo inalenga kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wateja kupitia maboresho yatakayofanywa na wataalamu wa ndani na nje ya nchi.

"Tunafahamu kuwa hatua hii inaweza kuleta usumbufu kwa wateja wetu, lakini ni muhimu kwa ajili ya kuboresha huduma na kuhakikisha usalama wa miamala," imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.

Katika kipindi hicho cha siku tatu, huduma zote za benki hazitapatikana kwa namna yoyote ile. Hii inajumuisha huduma katika matawi yote ya CRDB, mawakala wa benki (CRDB Wakala), mashine za kutolea pesa (ATM), pamoja na huduma za kidijitali kama SimBanking, Internet Banking, na miamala ya benki kupitia mitandao ya simu.

Aidha, benki hiyo imefafanua kuwa huduma zitaanza kuzimwa rasmi kuanzia saa sita usiku wa kuamkia Septemba 5, ambapo kutakuwa na kukatika kwa huduma kwa muda wa saa mbili, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya maboresho hayo.

CRDB imetoa wito kwa wateja wake kupanga shughuli zao mapema kabla ya tarehe hizo ili kuepuka usumbufu. Aidha, imesisitiza kuwa huduma zitarudi kama kawaida kuanzia Jumatatu, Septemba 8, mara baada ya maboresho kukamilika.




Chapisha Maoni

0 Maoni