WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa ametoa wito kwa watunza
kumbukumbu wote nchini kuzingatia maadili ya kazi, kudumisha uadilifu na
kulinda usiri wa taarifa zote zinazohifadhiwa kwani taarifa hizo ni nyenzo
muhimu ya usalama wa Taifa na maendeleo ya nchi.
Amesema kuwa Chama Cha Menejimenti ya Kumbukumbu na Nyaraka
Tanzania (TRAMPA) kinabeba dhamana kubwa ya kuhakikisha nyaraka na kumbukumbu
zote muhimu za Serikali pamoja na taasisi binafsi zinatunzwa kitaalamu na
zinahifadhiwa.
Ametoa wito huo leo Jumatano (Agosti 27, 2025) wakati
alipofungua Mkutano Mkuu wa 13 wa Chama Cha Menejimenti ya Kumbukumbu na
Nyaraka Tanzania, uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Diamond Jubilee
jijini Dar es Salaam.
“Utunzaji sahihi wa nyaraka na kumbukumbu ni uti wa mgongo
wa uwajibikaji, historia, na utawala bora. Bila masjala madhubuti, Taifa letu
lingeweza kukabiliwa na changamoto kubwa za upotevu wa taarifa, ucheleweshaji
wa maamuzi, na hatimaye kurudisha nyuma juhudi za maendeleo.”
Aidha, Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa TRAMPA inapaswa
kuendelea kuchochea uwajibikaji, utawala bora pamoja na kukuza utaalamu na
weledi wa usimamizi wa nyaraka na kuhimiza utoaji wa mafunzo na miongozo ya
kitaalamu ili kuhakikisha nyaraka zote zinatunzwa kwa viwango vya juu vya
usiri, usahihi na usalama.
Kadhalika, Mheshimiwa Waziri Mkuu ameziagiza Taasisi zote za
Umma ambazo bado hazijaanza kutumia mfumo wa e-Office zihakikishe zinaanza mara
moja kutumia teknolojia hiyo ya kisasa kwani Serikali imewekeza katika mifumo
hiyo kwa lengo la kupunguza matumizi ya karatasi, kuongeza kasi ya mawasiliano
na kulinda siri za Serikali.
“Kupitia mfumo wa Ofisi Mtandao (e-Office), Wizara, Idara,
Wakala na Taasisi mbalimbali za Serikali zimewezeshwa kutumia mifumo ya kisasa
ya kidijitali inayorahisisha upatikanaji wa kumbukumbu, kuongeza uwazi na
kupunguza ucheleweshaji wa huduma.”
Wakati huo huo, Waziri Mkuu amesema kuwa Serikali ya Awamu
ya Sita, imeendelea kulipa jumla ya shilingi bilioni 252.76 za malimbikizo ya
mishahara ya watumishi 150,647 pamoja na kulipa shilingi bilioni 33.29 za
malimbikizo ya mishahara ya wastaafu 10,022.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejiementi
ya Utumishi wa Umma ma Utawala Bora, George Simbachanwene amesema kuwa Serikali
imeeendelea kutoa ajira kwa watumishi wa umma wakiwamo watunza kumbukumbu.
“Katika mwaka 2024-2025 kada hii tu ajira mpya zilizotolewa ni 965
waliopandishwa cheo ni 1,237, kuwabadilishia kada watumishi 59
(Recategorization) pamoja na kulipa malimbikizo ya mishahara kiasi cha shilingi
milioni 204.6”
Amesema kuwa Serikali inatambua mchango kada ya Menejimenti
ya Kumbukumbu na Nyaraka katika ustawi wa utumishi wa umma na wakati wote
itaendelea kutoa ushikiano kwa kada hiyo ili kuendelea kufanikisha masuala
mbalimbali ya kiutumishi.
Naye, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi
na Utawala Bora wa Serikali ya
Mapinduzi Zanzibar, Mhe. Haroun Ali Suleiman amepongeza wanachama wa chama
hicho kwa kazi kubwa wanayoifanya ya utunzaji wa siri za ofisi kwa maslahi ya
Taifa. “Pamoja na hili ninawapongeza sana kwa uamuzi wenu mzuri wa ujenzi wa
jengo kubwa na la kisasa”.
Amesema kuwa, kwa kutambua umuhimu wa kada hiyo, Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar inajenga jengo kubwa na la kisasa la utunzaji kumbukumbu ambalo
litazinduliwa hivi karibuni. “Pia Serikali kwasasa inajenga majengo mapya ya
kisasa na katika hili tunazingatia uwepo wa ofisi nzuri za watunza kumbukumbu.”
Awali, Mwenyekiti wa TRAMPA, Devota Mrope amempongeza Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa
anayoifanya katika sekta mbalimbali iliwemo katika kada ya Menejimenti ya
Kumbukumbu na Nyaraka.
“Rais Dkt. Samia amekuwa mwana TRAMPA namba moja, amepigania
maslahi ya watumishi wa umma ikiwemo sisi
mwana TRAMPA, ametoa ajira nyingi katika kipindi kifupi ikiwemo kwa wanataaluma wa kada hii ya Menejimenti ya
kumbukumbu na nyaraka, amefanyia kazi changamoto zetu kwa kiasi kikubwa.”
Katika mkutano huo, TRAMPA wamemkabidhi Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan gari la kubebea wagonjwa (Ambulance) ambayo wamesema yeye mwenyewe ataamua iende wapi kwa ajili ya matumizi kwenye sekta ya afya.





0 Maoni