Wanaume waaswa namna bora ya kushughulikia utasa

 

Daktari Bingwa wa Masuala ya Uzazi, Dkt. David Mwesigye, amewataka wanaume kuacha tabia ya kuwalaumu au kuwaacha wake zao pale wanaposhindwa kupata mtoto, akisisitiza kuwa tatizo la utasa linaweza kumpata mwanamume au mwanamke.

Dkt. Mwesigye, ambaye ni mtaalamu wa Kliniki ya Uzazi nchini Rwanda, alitoa ushauri huo wakati wa semina ya waandishi wa habari kutoka nchi mbalimbali za Afrika, iliyoandaliwa na Taasisi ya Merck Foundation kwa kushirikiana na Baraza la Habari Tanzania (MCT).

"Nawashauri wanaume wasikimbilie kuwaacha wake zao wanaposhindwa kupata watoto. Wengine wamewaacha wake zao wakidhani wao si tatizo, lakini baadaye wanashangaa kuona wake hao wamepata watoto kwenye ndoa nyingine. Kumbe shida ilikuwa kwa mwanaume," alisema Dkt. Mwesigye.

Alisema badala ya kufunga ndoa nyingine, wanaume wanapaswa kutafuta ushauri wa kitaalamu kwani gharama za vipimo na tiba ni nafuu ikilinganishwa na gharama za kuvunja ndoa na kuanzisha nyingine.

Uelewa mdogo wa masuala ya uzazi wawakandamiza wanawake

Dkt. Mwesigye alieleza kuwa kutokana na uelewa mdogo wa masuala ya uzazi barani Afrika, wanawake wengi hujikuta wakibebeshwa lawama za kukosa mtoto, mara nyingi wakihusishwa na utoaji wa mimba wa zamani, ilhali sababu halisi zinaweza kuwa nyingi.

Sababu kuu za utasa

Miongoni mwa sababu alizozitaja kuwa chanzo cha utasa ni pamoja na:

Lishe duni au uzito kupita kiasi.

Magonjwa ya zinaa yasiyotibiwa.

Maambukizi ya mfumo wa uzazi.

Upungufu wa kinga mwilini (kama virusi vya UKIMWI).

Alitaja pia magonjwa ya zinaa yanayosababisha utasa kwa wanawake kuwa ni Klamidia (Chlamydia) na Kisonono (Gonorrhea), ambayo huathiri mfumo wa uzazi.

"Kwa Afrika, takriban asilimia 85 ya wanawake wanaopata huduma za utasa huwa wameathiriwa na maambukizi, ikilinganishwa na asilimia 33 katika maeneo mengine ya dunia," alisema.

Bodaboda na matumizi ya kompyuta yapewa tahadhari

Kwa upande mwingine, Dkt. Mwesigye alionya kuwa wanaume wanaoendesha pikipiki kwa muda mrefu, maarufu kama bodaboda, wako katika hatari ya kushuka kwa uzalishaji na ubora wa mbegu za kiume kutokana na joto linalotokana na injini.

"Korodani hufanya kazi vizuri katika joto la chini. Joto linalozalishwa na injini linaweza kuathiri uzalishaji wa mbegu," alisema.

Aliwataka wanaume kuepuka kuoga maji ya moto kwa kutumia hot tub, kutumia steam bath, kupakata kompyuta (laptop) mapajani kwa muda mrefu, pamoja na mazingira yenye sumu za viwandani.

Lishe na mtindo wa maisha bora vinasaidia uzazi 

Ili kuimarisha afya ya uzazi, Dkt. Mwesigye alishauri kufanya mazoezi ya wastani, kula mlo kamili, kuepuka pombe, sigara, dawa za kulevya na kupunguza vinywaji vyenye kafeini. Aliongeza kuwa msongo wa mawazo ni moja ya sababu zinazochangia matatizo ya uzazi.

Ukeketaji na ndoa za utotoni vyatajwa kuchangia utasa

Dkt. Francisca Bwalya kutoka Zambia alizungumzia mila ya ukeketaji na ndoa za utotoni, ambazo bado zinaendelea katika familia nyingi masikini barani Afrika, kuwa chanzo kingine cha utasa.

"Zaidi ya wanawake na wasichana milioni 200 duniani wamekeketwa, hasa katika nchi za Kusini mwa Afrika na mataifa ya Kiarabu. Ukeketaji husababisha maambukizi na matatizo ya mfumo wa uzazi," alisema Dkt. Bwalya.

Aliongeza kuwa ndoa za utotoni huwalazimisha wasichana kuingia kwenye majukumu ya uzazi kabla miili yao haijakomaa, jambo ambalo huongeza hatari ya matatizo ya kiafya, ikiwemo utasa.

Jamii yatahadharishwa dhidi ya lugha za unyanyapaa

Afisa Lishe kutoka Kenya, Bi. Christine Nguku, alitoa wito kwa jamii kuacha kutumia lugha za unyanyapaa dhidi ya wanawake wanaokosa watoto, kama vile:

“Lini utazaa?”, “Nizalie wajukuu wangu”, “Hujui uchungu wa mwana kwa kuwa hujazaa”.

Alivitaka vyombo vya habari kuwa mstari wa mbele katika kuelimisha jamii kwa mtazamo chanya na kumwonyesha mwanamke anayepitia changamoto za utasa kama mtu jasiri, si mnyonge.

Mifano ya mataifa yanayotoa msaada wa tiba

Katika nchi kama Israeli, serikali hutoa huduma za bure kwa wanandoa wenye changamoto ya utasa hadi watoto wawili.

Canada na Uingereza, kwa upande wao, hutoa ruzuku ya serikali kwa watu wanaotafuta huduma za uzazi kwa njia ya kitaalamu.

Chapisha Maoni

0 Maoni