Waandishi wa habari
nchini wametakiwa kutumia taaluma yao kuhamasisha na kuelimisha wananchi
kujitokeza kwa wingi kupiga kura ifikapo tarehe 29 Oktoba, 2025.
Wito huo umetolewa na Mwenyekiti
wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji wa Mahakama ya Rufaa Jacobs
Mwambegele, wakati akifungua Mkutano wa Kitaifa kati ya Tume na Waandishi wa
Habari kuhusu Uchaguzi Mkuu, uliofanyika tarehe 2 Agosti, 2025 katika ukumbi wa
Mlimani City, jijini Dar es Salaam.
Mhe. Jaji Mwambegele
amesema vyombo vya habari vina mchango mkubwa katika kuhakikisha wananchi
wanashiriki kikamilifu kwenye uchaguzi mkuu kwa kuwapatia taarifa sahihi na kwa
wakati kuhusu masuala mbalimbali ya uchaguzi.
Ameeleza kuwa waandishi
wa habari wana wajibu mkubwa wa kutumia taaluma yao kuwaelimisha wananchi
waliojiandikisha kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, ili waweze kujitokeza
kwa wingi kushiriki zoezi la kupiga kura.
Kwa upande wake,
Mkurugenzi wa Uchaguzi Bw. Kailima Ramadhani amewakumbusha wanahabari wajibu
wao wa kuhakikisha vyama vya siasa na wagombea wanapata nafasi ya kufikisha
ujumbe wao kwa wapiga kura katika kipindi cha kampeni.
Aidha, Bw. Kailima
amewataka wanahabari kutoa taarifa sahihi kwa umma na kuepuka kusambaza taarifa
potofu katika hatua zote za mchakato wa uchaguzi, huku akisisitiza umuhimu wa
kuzingatia sheria na maadili ya taaluma ya habari.
Amewahimiza waandishi hao
kutumia kalamu na nyenzo zao kueneza ujumbe wa amani kabla, wakati na baada ya
uchaguzi, ili kulinda mshikamano wa kitaifa na kuimarisha misingi ya
demokrasia.
Pia amewaasa kuepuka
kuchapisha au kurusha habari zinazoweza kuwavunja moyo wananchi na kuwafanya
waone kama hakuna umuhimu wa kushiriki katika uchaguzi, iwe ni kama wapiga kura
au wagombea.
Mkutano kati ya Tume na
Waandishi wa Habari ni sehemu ya mfululizo wa mikutano ya wadau mbalimbali
ambayo Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi imekuwa ikiitisha katika maandalizi ya
kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025.
Mikutano hiyo ilianza
tarehe 27 Julai 2025 kwa kukutana na Viongozi wa Vyama vya Siasa, ikafuatiwa na
mkutano na Wawakilishi wa Asasi Zisizo za Kiserikali kisha Wawakilishi wa
Wanawake, Vijana na Watu Wenye Ulemavu, pamoja na Wahariri wa Vyombo vya
Habari.
Mfululizo huu wa mikutano
unatarajiwa kuhitimishwa tarehe 4 Agosti 2025, baada ya mkutano na Waandaji wa
Maudhui Mtandaoni, utakaofuatiwa na mafunzo kwa Wahariri na Waandishi wa
Habari.
0 Maoni