Naibu Katibu Mkuu
Ofisi ya Rais – TAMISEMI (Afya), Profesa Tumaini Nagu, amewataka Maafisa Afya
wa Mikoa na Halmashauri kote Tanzania Bara kuhakikisha wanachukua hatua
madhubuti kupunguza magonjwa ya mlipuko, huku akiwasisitiza kuweka kipaumbele
kwenye maeneo yenye changamoto ili yafanyiwe kazi kwa haraka.
Profesa Nagu alitoa
kauli hiyo juzi jijini Mwanza wakati wa kufunga mkutano wa mwaka wa tathmini ya
utekelezaji wa huduma za afya na usafi wa mazingira kwa mikoa na halmashauri
zote, uliofanyika katika Ukumbi wa Rock City Mall kuanzia Julai 2 hadi Julai 5,
2025.
Akizungumza wakati wa
kufunga mkutano huo, Profesa Nagu alisema ni muhimu kwa maafisa afya kutumia
mkutano huo kwa kutoa taarifa sahihi na kwa wakati ili kusaidia katika
kudhibiti magonjwa ya mlipuko ambayo yamekuwa tishio kwa afya ya umma.
“Ni muhimu sana kuwa
na taarifa za wakati na sahihi kuhusu changamoto zinazojitokeza ili hatua
zichukuliwe mapema. Hii ndiyo njia pekee ya kuzuia milipuko ya magonjwa
isisambae zaidi,” alisema Prof. Nagu.
Mkutano huo ulilenga
kutathmini hali ya utoaji huduma za afya na usafi wa mazingira, kubaini
mafanikio yaliyopatikana, changamoto zilizopo na maeneo yanayohitaji ubunifu
ili kuboresha huduma hizo kwa jamii.
Kwa upande wake,
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Dkt. Jesca Lebba, aliwataka waganga wakuu wa
mikoa kushiriki kikamilifu katika vikao kama hivyo kwa lengo la kuimarisha
ushirikiano kati yao na maafisa afya.
“Tukiendelea
kushirikiana kwa karibu kama wataalamu wa afya, tutafanikiwa kuondoa changamoto
nyingi zinazokumba sekta hii, hasa kwenye afua za tiba na usafi wa mazingira,”
alisema Dkt. Lebba.
Aidha, Mratibu Mkuu
wa mkutano huo, Seleman Yondu, aliwakumbusha washiriki kuzingatia sheria,
taratibu na miongozo ya kazi ili kuhakikisha matokeo chanya katika utekelezaji
wa majukumu yao. Alisisitiza umuhimu wa ubunifu, bidii na weledi katika
utendaji wa kila siku.
Kauli mbiu ya mkutano
huo ilikuwa: “Utekelezaji wa afua za afya na usafi wa mazingira ni msingi wa
kinga endelevu dhidi ya magonjwa na ustawi wa jamii.”
Mkutano huu wa siku
nne umejikita katika kutoa fursa kwa maafisa afya kubadilishana uzoefu na
kujifunza mbinu mpya zitakazosaidia kuimarisha huduma za afya nchini.
0 Maoni