Mamlaka ya Usimamizi wa
Wanyamapori Tanzania (TAWA) kwa kushirikiana na Msakuzi Sports Promotion leo
Julai 12,2025, imezindua rasmi msimu wa kwanza wa mbio za riadha zinazojulikana kama
"Msakuzi Pande Game Reserve Marathon" zilizofanyika katika Hifadhi ya
Pande iliyopo jijini Dar es Salaam.
Akizungumza kwa niaba ya
Waziri wa Maliasili na Utalii, Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa la
Tanzania, Dkt. Noel Lwoga amesema lengo kuu la mbio hizi ni kuunga mkono juhudi
za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Dkt Samia Suluhu Hassan za
kutangaza na kuhamasisha utalii.
"Sote ni mashahidi
juhudi hizi zimeweza kuongeza idadi ya watalii wa nje na ndani, ukiangalia
idadi ya watalii wa ndani wameongezeka kutoka takribani watalii laki tisa mwaka
2021 hadi watalii takriban Milioni tatu kwa mwaka 2024," amesema Dkt.
Lwoga
Sambamba na hilo, Dkt.
Lwoga amesema mbio hizi zimejikita pia katika kuhamasisha jamii kushiriki
kwenye michezo ili kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza.
"Mbio hizi zina tija
sio kwenye michezo pekee ila zinahamasisha utalii na kujenga afya zetu, na
hakika zimefanikiwa tumekimbia, tumeburudika, tumeona wanyamapori mbalimbali,
unakimbia huku unavuta hewa safi," ameongeza Dkt. Lwoga.
Kwa upande wake, Kamanda
wa Hifadhi ya Pande, Dorothea Massawe amesema mbio za Msakuzi Pande Game
Reserve zimejumuisha washiriki takribani 300 na zimeambatana na shughuli
zingine za utalii kama vile mlo wa porini (nyamapori choma) na kuona
wanyamapori mbalimbali wanaopatikana katika Hifadhi hiyo wakiwemo Simba, Chui,
Pundamilia, Mbuni, Kasongo na pundamilia.
Naye, Katibu wa Msakuzi
Sports Promotion, Peter Mpulila ameushukuru uongozi wa TAWA kwa ushirikiano
walioupata hadi kukamilika kwa mbio hizo.
Kadhalika, Bw. Mpulila
ameongeza kwa mbio hizi zimejikita katika kupambana na magonjwa yasiyoambukiza
na kutangaza vivutio vya utalii vilivyo ndani ya nchi.
Na. Joyce Ndunguru- Dar
es Salaam
0 Maoni