Wafanyabiashara wa Soko la Kariakoo wamehakikishiwa kuwa Serikali imejenga upya lililokuwa soko dogo na kukarabati soko lililoungua kwa ajili ya manufaa ya kiuchumi ya Watanzania wote bila ubaguzi.
Kauli hiyo imetolewa na
Meneja Mkuu wa Shirika la Masoko ya Kariakoo CPA Ashraph Abdulkarim jana Julai 28,
2025 katika ukumbi wa soko la Machinga
Dar es Salaam wakati alipofanya kikao na wafanyabiashara wa Soko hilo
wanaotarajiwa kurejeshwa ndani ya soko.
CPA Abdulkarim alisema
lengo la kikao hicho ni kuwapa mrejesho na taarifa juu ya maendeleo ya mradi na
hatua zinazofanyika na Shirika kuwapanga wafanyabiashara ndani ya soko.
“Ninawaahidi kuwa
tutasikiliza kila mfanyabiashara na kutatua changamoto zake kwa mujibu wa
sheria na taratibu za upangishaji za Serikali ili kila mtu apate haki yake na
kunufaika na uwepo wa soko la Kariakoo,” alisema CPA Abdulkarim.
Meneja Mkuu huyo
amewasihi wafanyabiashara hao kuwa mabalozi wa soko hilo kwa kuelezea mazuri
yanayofanywa na Serikali ili wananchi wanufaike.
Kikao hicho kilihusisha
wafanyabiashara wa pembejeo, viuatilifu, mizani, cherehani, vifungashio, nafaka
na viungo vikavu ambao wamepangiwa sakafu ya tatu, nne na tano soko jipya huku
baadhi yao wakiwa na maoni ya kuboresha mchakato kuelekea ufunguzi wa soko
hilo.
Emanuel Mbise, Mwenyekiti
wa wauza pembejeo za kilimo alisema Shirika liweke wazi mikataba wa upangishaji
pamoja na kutorusu biashara za pembejeo kuchanganywa na bidhaa zingine ili
kulinda walaji.
Naye Abdala Bashiru
Selemani alitoa rai kwa uongozi wa Shirika kuwapanga waliokuwa wafanyabiashara
soko lililoungua ambao sasa watapangiwa soko jipya sakafu ya nne ili wawe na
uhakiki wa biashara badala ya kuchanganywa na makundi mengine.
Ashraph Waziri
mfanyabiashara ya nafaka aliomba Serikali ifikirie kuwapa muda wa matazamio na
nafuu ya kodi wafanyabiashara wote ambao walipata hasara ya mali zao
kutekeketea kwenye tukio la moto la 10 Julai 2021 kwa kuwa hakuna fidia yoyote
hadi sasa waliopata.
Akijibu hoja na maswali
hayo Meneja Mkuu CPA Abdulkarim alisema wataziratibu hoja hizo kuzitafutia
majawabu ikiwemo kuongeza nafasi za majadiliano na wafanyabiashara wakati huu
wa kuelekea ufunguzi wa Soko la Kariakoo ikiwemo kutoa elimu ya bima ya majanga
ikiwemo moto.
Serikali ya Awamu ya Sita
chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ilitoa fedha shilingi Bilioni 28.03
ambazo zilifanya kazi ya kujenga soko jipya na kukarabati la zamani hatua
inayofanya soko kuwa la kisasa ambapo maeneo ya biashara yameongezeka toka 1,662 mwaka 2021 hadi 1,907 na ajira
zaidi ya 4,000 zitazalishwa.
0 Maoni