WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameshiriki ufunguzi wa Mkutano
wa siku mbili wa Maafisa Watendaji Wakuu barani Afrika ulioanza leo Mei 12,
2025, katika ukumbi wa hoteli ya Sofitel jijini Abidjan, Ivory Coast.
Mheshimiwa Majaliwa amemwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu
Hassan katika mkutano huo ambao umefunguliwa na Rais wa Ivory Coast, Alassane
Ouattara na kuwakutanisha Maafisa Watendaji Wakuu zaidi ya 3000, wawekezaji na
Wakuu wa Nchi na Serikali.
Akizungumza na washiriki wa jukwaa hilo, Rais Ouattara
amesema kuwa mkutano huo utawawezesha washiriki kujadili changamoto
zinazolikabili bara la Afrika na kutoa majawabu ya changamoto hizo katika
maeneo ya uchumi, fedha, mazingira na biashara.
Ameongeza kuwa ili bara la Afrika liweze kuendelea
kuimarisha uchumi wake, viongozi wanapaswa kuendelea kuweka na kutekeleza
mikakati ya kuongezea thamani mazao yanayozalishwa.
Wakati huohuo, Waziri Mkuu ameshiriki Mjadala wa Marais
ulioendeshwa na Mwandishi wa Kujitegemea wa CNN, Larry Madowo na kuwashirikisha
Marais wa Afrika Kusini, Rwanda, Mauritania na Makamu wa Rais wa Ivory Coast.
Akichangia mjadala huo, Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika
Kusini amesema suala la amani na usalama Mashariki mwa Congo (DRC) limepitia
hatua kadhaa za mazungumzo na mashauriano hadi kufikia hatua ya majeshi kuanza
kujiondoa kwenye eneo hilo.
Amesema mazungumzo ya Nairobi, Rwanda na Qatar yalifanyika na yamesaidia kujenga msingi imara wa hatua iliyofikiwa hivi sasa lakini zaidi ni kutokana juhudi za wadau wengine wanaotaka amani wakiwemo viongozi wa dini.
“Kwenye masuala kama haya ni lazima tutambue kuwa matatizo
ya Afrika yatapata suluhu za Kiafrika na hili ni bara letu kwa hiyo tunao
wajibu wa kushughulikia matatizo yetu na siyo kutafuta ufumbuzi kutoka nje,”
alisema na kushangiliwa.
Akichangia swali ni kwa jinsi gani bara la Afrika linaweza
kujisimamia kiuchumi kwa kutumia rasilimali zake, Rais Paul Kagame wa Rwanda
alisema kuna umuhimu wa sekta binafsi kuwezeshwa ili iweze kuchangia ukuaji wa
uchumi barani humo.
“Hatuwezi kuhimiza sekta binafsi ishiriki kwenye ukuzaji wa
uchumi kama Serikali zetu hazitawawezesha kwa kuwapa vivutio ikiwemo sera,
sheria, kanuni pamoja na utawala bora. Nazungumza hivyo kwa sababu kuna mambo
huwa tunakubaliana kwenye vikao lakini utekelezaji wake unachukua muda mrefu
sana, na hii inakarahisha,” alisema.
“Hatuwezi kuacha hali hii iendele kwa sababu nguvu tunayo,
maono tunayo, rasilmali tunazo na tunazo njia wa kutekeleza hayo,” alisema.
Naye Rais wa Mauritania, Mohamed Cheikh El-Ghazouani alisema
maendeleo ya kijamii na kiuchumi yanaweza kukua kupitia ushirikiano baina ya
sekta binafsi na umma wwnye nia ya kujiletea maendeleo.
Baadaye leo jioni, Waziri Mkuu atashiriki mjadala ukaojumuisha mawaziri wakuu wanne kutoka Tanzania, Ivory Coast, Guinea na Cameroun.




0 Maoni