Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus
Balile ameshauri waandishi wa habari kuwa na alama za utambuzi wakati wa
kuripoti kesi ya Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema),
Tundu Lissu.
Akizungumza na waandishi wa habari leo tarehe 2 Mei 2025,
katika Ofisi ya taasisi hiyo zilizopo Mtaa wa Mtendeni jijini Dar
es Salaam Balile alisema, miongoni mwa alama hizo ni kuvaa jaketi la uandishi wa
habari na kitambulisho cha kazi.
"Baada ya zile purukushani pale mahakamani, nikasema
haiwezekani mwandishi akazuiwa kufanya kazi yake."
"Nilikutana na Afande Jumanne Muliro (Kamanda wa Polisi
Kanda Maalum ya Dar es Salaam) na tukakubalia kuzuia waandishi Kisutu sio jambo
jema. Tukakubaliana siku ya kesi ya Lissu tarehe 6 Mei waingie wote lakini kuwe
na utambuzi," alisema Balile.
Balile alisema, mwandishi hapaswi kuzuiwa kufanya kazi yake
ya kukusanya, kuchakata na kuhabarisha umma.
Hata hivyo alisema, wanahabari wanapaswa kufika mahakamani
mapema kwa kuwa, chumba kikijaa hawatopata nafasi.
Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari Dar es Salaam
(DCP), Bakari Kimwanga alisema, wanahabari wanapaswa kuhakikisha wanakuwa
salama wakati wa kazi.
"Jambo la usalama ni la kwanza kisha kazi (habari), jukumu la usalama ni lako mwanahabari," alisema Kimwanga.


0 Maoni