WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Tanzania ni miongoni mwa
nchi zinazofanya kazi kwa karibu sana na sekta binafsi ili kukuza uchumi na
kuleta maendeleo kwa wananchi wake.
Ametoa kauli hiyo jana jioni (Jumatatu, Mei 12, 2025) wakati
akishiriki mjadala uliojumuisha mawaziri wakuu wanne kutoka Tanzania, Ivory
Coast, Guinea na Cameroun katika moja ya vikao vya jukwaa la siku mbili la
Maafisa Watendaji Wakuu barani Afrika ambao unaendelea hoteli ya Sofitel jijini
Abidjan, Ivory Coast.
Waziri Mkuu Majaliwa ambaye anamwakilisha Rais Dkt. Samia
Suluhu Hassan katika jukwaa hilo alitumia fursa hiyo kuelezea namna ambavyo
Serikali ya Tanzania imekuwa ikiishirikisha sekta binafsi kwa kufungua milango
ya fursa mbalimbali ili iweze kutumika na kuleta manufaa katika nchi.
“Serikali ya Tanzania inafanya kazi kwa karibu na Tanzania
Private Sector Foundation, vyama vya wafanyakazi, vya waajiri na wenye viwanda
na pia inawapa fursa ya kujenga mshikamano kwa kufanya kazi na Serikali. Pia
imefungua milango kwa wawekezaji kutoka ndani ya nchi, nje ya bara la Afrika na
duniani kwa ujumla ili kukuza uchumi wa ndani.”
Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwaeleza faida za African
Continental Free Trade Area (AfCFTA) na jinsi ambavyo Tanzania imetumia fursa
hiyo kuimarisha miundombinu ya reli na bandari kutokana na nafasi yake
kijiografia. “Tumeimarisha bandari za Tanga, Dar es Salaam na Mtwara na pia
tuna mpango wa kuanza ujenzi wa bandari ya Bagamoyo,” alisema.
Amesema Tanzania inaendelea na ujenzi wa reli ya kisasa ya
SGR ili kuziunganisha nchi za Congo, Rwanda na Burundi, pia kuna reli ya TAZARA
inayokwenda Zambia. Tumeimarisha usafiri wa anga na barabara ili kuwawezesha
wanaokuja kuwekeza Tanzania wapate urahisi wa huduma muhimu.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano
wa Kimataifa, Bw. Cosato Chumi alisema kwenye jukwaa hilo limetoa fursa ya
kuithibitishia dunia azma ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuendeleza
diplomasia ya uchumi na kuifungua Tanzania kiuchumi.
“Washiriki wengi hapa wanaelezea mafanikio ya mkutano mkubwa
uliofanyika Januari, 2025 wa Energy Summit, na mikutano mingine mikubwa ambayo
nchi yetu imeiandaa. Pia tumepata taarifa kuwa Burkina Faso wanataka kuja
nchini kujifunza kuhusu uendeshaji wa hospitali ya Jakaya Kikwete ili nao
waweze kujenga hospitali kama hiyo.”
Naye Balozi wa Tanzania nchini Nigeria ambaye ni mwakilishi
wa Tanzania nchini Ivory Coast, elestine Kakele amesema ushiriki wa Tanzania
kwenye jukwaa hilo unasaidia kutangaza fursa ambazo Tanzania inazo na hasa
kwenye zao la mkonge. “Hii ni nafasi muafaka kwa sekta binafsi kuchukua nafasi
yake kama injini ya kusukuma maendeleo.”
Naye Msajili wa Hazina, Bw. Nehemia Mchechu alisema uwepo wa
Tanzania kwenye jukwaa hilo umetoa nafasi ya kukutana na wadau mbalimbali wa
maendeleo barani Afrika na hivyo kutoa fursa kwa nchi kujitangaza ili kuvutia
uwekezaji ambao utawezesha kuiinua nchi kiuchumi.
“Tunaamini kwenye vikao hivi wameendelea kuijua Tanzania na fursa zake zilizoko kwenye uwanda wetu wa logistics, katika madini, kilimo na hata katika sekta ya fedha.”




0 Maoni