Katika kuhakikisha mazingira ya hifadhi na shoroba za Wanyamapori yanabaki salama kwa uhifadhi endelevu, Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro (NCAA) imeendelea kushirikiana kwa karibu na wananchi wa vijiji vinavyopakakana na hifadhi ya Ngorongoro kupambana na mmea vamizi hatari uitwao Gugu Karoti (Parthenium hysterophorus) ambao umeota baadhi ya maeneo.
Hatua ya ushirikishaji
wa jamii ni sehemu ya mpango wa kitaifa wa kudhibiti mimea vamizi nchini,
hususan katika maeneo ya yaliyohifadhiwa na kuzilinda shoroba muhimu
zinazounganisha mifumo ya ikolojia kama vile shoroba ya Upper Kitete
inayounganisha hifadhi za Ngorongoro, ziwa Manyara na Tarangire.
Afisa Uhifadhi darala
la Kwanza Gregory Mtega kutoka NCAA
akiongoza wananchi wa Kijiji cha Upper Kitete na baadhi ya wataalam
ameeleza kuwa operesheni ya kung’o gugu
karoti imefanyika kwa mafanikio makubwa kupitia ushirikiano kati ya NCAA,
Halmashauri ya Wilaya ya Karatu na shirika la PAMS na kuongeza kuwa juhudi hizo
zinaendelea katika vijiji vingine vinavyopakana na hifadhi kwa ajili ya
kuhifadhi uoto wa asili, malisho ya mifugo, na maisha ya wanyamapori.
“Tumekuwa na
utaratibu wa kutoa elimu ya uhifadhi shirikishi kwa wananchi wa vijiji
vinavyozunguka hifadhi, NCAA kila mwaka tunatoa miche ya miti bure wananchi
wapande kwenye maeneo yao, tunagawa mizinga ya Nyuki kuwainua kiuchumi na
kupambana na Wanyama wanaoingia kwenye maeneo hayo, pamoja na programu hizo
tumeamua pia kuwahusisha kwenye kung’oa mimea vamizi ili kulinda mfumo wa
ikolojia kuwa imaraa, kuimarisha nyanda za malisho na kuwa na uhifadhi endelevu.”
Mtega ameongeza kuwa
Gugu Karoti ni mmea unaosababisha uharibifu mkubwa wa mazingira kwa kuwa
unazaliana kwa kasi (mbegu zaidi ya 40,000 kutoka mmea mmoja!), na ni tishio
kwa wanyamapori, mifugo, na hata kilimo cha wananchi hivyo mamlaka imewekeza
juhudi za kutosha kukabiliana nalo kw akutumia njia mbalimbali.
Afisa Wanyamapori wa
Halmashauri ya Wilaya ya Karatu, Kornelio Lengai, amepongeza ushirikiano wa
NCAA na kueleza kuwa mmea huo umekuwa kikwazo kwa uzalishaji wa chakula na
maisha ya wakazi wa vijiji vinavyozunguka hifadhi hivyo Jitihada za NCAA
kushirikiana na wadau mbalimbali ni ishara nzuri katika uhifadhi endelevu kwa
vizazi vijavyo.
Kwa upande wake,
Emanuel Siriri, mkazi wa kijiji cha Upper Kitete, ameishukuru NCAA kwa
kuendelea kutoa elimu na kuwashirikisha wananchi wa kijiji hicho ambapo
jitihada hizo si tu zinaleta matumaini bali zimefungua fursa za kiuchumi kwa
vijana kupitia kazi za udhibiti wa mmea huo ambao unapodhibitiwa unaboresha
shughuli za kilimo na kupata mazao ya kutosha.
Na. Mustapha Seifdine - Karatu
0 Maoni