Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Ridhiwani Kikwete amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Nchi ya Uswisi nchini Tanzania, Nicole Providoli, katika Ofisi ya wizara hiyo iliyopo Jijini Dar es Salaam alipofika kujitambulisha.

Katika kikao hicho kilichofanyika jana, Mhe. Ridhiwani alimshukuru Balozi Providoli kwa ushirikiano uliodumu wa zaidi ya miaka 63 baina ya nchi hizo mbili na kumuhakikishia kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatambua mchango mkubwa wa Serikali ya Uswisi kupitia shirika la Swiss Aid na ushirikiano unaoendelea katika nyanja mbalimbali ikiwemo sekta ya afya, maendeleo ya jamii pamoja na masuala ya ukuzaji ujuzi kwa vijana.

Pia, Mhe. Ridhiwani amepongeza na kuushukuru ubalozi wa Uswisi kwa mchango wake katika kufanikisha kukamilika Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Vijana (2007), Toleo la Mwaka 2024 ambayo inatoa mwongozo kwa vijana na wadau wengine kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya kijamii, kisiasa na kiuchumi; na utayari wao kusaidia usambazaji wa Sera hiyo kuwafikia Wadau.