Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Raisi-Tamisemi anayeshughulikia Miundombinu, Mhandisi Rogatus Mativila amezitaka halmashauri zote nchini kuhakikisha zinasimamia kikamilifu zoezi la usafi wa barabara, akisisitiza kuwa serikali imewekeza fedha nyingi katika ujenzi wa miundombinu hiyo muhimu.
Mhandisi Mativila amesema hayo mkoani Iringa wakati wa ukaguzi wa ujenzi wa
barabara ya Wenda–Mgama Km.19 inayojengwa na TARURA kupitia mradi wa RISE kwa
gharama ya shilingi bilioni 29.7 ambayo imefikia asilimia 99 ya utekelezaji.
Mhandisi Mativila amesema usimamizi mzuri wa barabara
unahitajika ili kuhakikisha barabara hizo zinadumu na kuleta manufaa
yaliyokusudiwa kwa wananchi.
"Ni wajibu wa kila halmashauri kuhakikisha kuwa
barabara hizi zinatunzwa, hasa kwa kuhakikisha zinaendelea kuwa safi na salama
kwa matumizi. Hili ni jukumu la pamoja,” amesema Mativila.
Ameongeza kuwa uwepo wa barabara bora unachochea shughuli za
kiuchumi na kijamii kwa kuwawezesha wananchi kusafirisha bidhaa na huduma kwa
urahisi, hali inayosaidia kuongeza mapato ya halmashauri kupitia ushuru na tozo
mbalimbali.
Aidha, Mhandisi Mativila ametoa onyo kwa wakandarasi wazembe
wanaoshindwa kutekeleza miradi kwa viwango vilivyokusudiwa au kuchelewesha
kazi, akisema serikali haitasita kuwachukulia hatua kali.
“Serikali inataka kuona thamani ya fedha inaonekana katika
kila mradi na hatutavumilia uzembe unaokwamisha juhudi hizi za maendeleo,”
amesisitiza.
Mradi wa ujenzi wa barabara ya Wenda–Mgama ni sehemu ya jitihada za serikali kuboresha miundombinu ya vijijini kwa lengo la kuchochea ukuaji wa uchumi na kuimarisha ustawi wa wananchi.




0 Maoni