Jukwaa la
Malkia wa Nguvu la Clouds Media lilioanzishwa mwaka 2016 limeendelea kutimiza
lengo lake la kuhamasisha na kuunga mkono wanawake katika nyanja za
ujasiriamali, maendeleo ya kiuchumi na masuala mengine mbalimbambali ya kijamii
kwa kipindi cha miaka tisa sasa.
Akizungumza
Aprili 4, 2025 jijini Dar es Salaam wakati aliposhiriki katika sherehe za Tuzo
za Malkia wa Nguvu kwa mwaka 2025, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe.
Dkt. Doto Biteko amesema jukwaa hilo pia
hutambua, huthamini na husherehekea jitihada na michango ya wanawake
waliothubutu na kufanikisha maendeleo katika nyanja mbalimbali za kijamii,
uchumi na uongozi.
“ Tangu
kuanzishwa kwake, hadi sasa, jukwaa hili limekuwa ni chachu kubwa ya maendeleo
kwa wanawake na jami kwa ujumla. Naomba niwapongeze,
Clouds Media Group kwa kazi hii nzuri, ” Amesema Dkt. Biteko
Amesisitiza
“Kuanzisha na kuendeleza jukwaa hili ni kuunga mkono juhudi za Serikali na za
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan
za kuwawezesha wanawake kiuchumi,
kuongeza ushiriki wao katika sekta mbalimbali na kuhamasisha maendeleo
jumuishi. ”
Ametaja
mafanikio ya Serikali katika kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili
wanawake kijamii na kiuchumi sambamba na hatua kubwa ya kuhakikisha kuwa
mwanamke anakuwa sehemu ya maendeleo katika jamii kuwa ni fursa za elimu,
mazingira wezeshi ya kiuchumi, ushirikiano na jumuiya ya kimataifa, huduma bora
za afya pamoja na huduma za maji safi na nishati ya kupikia.
Aidha, Dkt.
Biteko ametoa rai kwa wadau wote muhimu kushirikiana na Serikali ili kutokomeza
changamoto zinazohitaji kutatuliwa ili kufungua fursa zaidi kwa wanawake.
Vilevile
ametoa wito kwa Clouds media na wanawake kushiriki kikamilifu katika kampeni
mbalimbali za Serikali mfano Kampeni ya Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia ili
kuhakikisha wanawake wanatumia Nishati Safi na kuwa na afya salama.
Fauka ya
hayo, Dkt. Biteko amewahakikishia kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na
wadau mbalimbali ili kufikia malengo tarajiwa.
Mkuu wa Mkoa
wa Dar es salaam, Mhe. Albert Chalamila amesema kuwa awali mwanamke hakuchuliwa
kama kiumbe anayeweza kuwa na mafanikio makubwa duniani, hata hivyo hali
imebadilika na sasa wanawake na Serikali mbalimbali duniani zimeonesha uwezo
mkubwa wa wanawake katika sekta mbalimbali.
Mwenyekiti wa
Kamati ya Malkia wa Nguvu kwa mwaka 2025, Lilian Masuka amesema kuwa Jukwaa la
Malkia wa Nguvu imeweza kuwatunuku tuzo wanawake zaidi ya 70, na kuwatambua
wanawake 300 katika shughuli zao.
Amesema
katika mwaka 2025 wanatarajia kutembelea mikoa mitano, hivyo wanaiomba Serikali
iwaunge mkono ili waweze kufika nchi nzima.
“ Kupitia
Rais Samia tumeona uwekezaji mkubwa na sera zilizoboreshwa ili kusaidia
wanawake kiuchumi,” amesema Masuka.
Ameongeza
kuwa wanawake wengi nchini bado wanatumia nishati isiyo safi ikiwemo mkaa,
hivyo ametoa wito huo ili waweze kutumia Nishati Safi ya Kupikia pamoja na
Serikali kuendelea kuwezesha mikopo rafiki kwa wanawake ili kuwawezesha kuwa na
uwezo wa kumiliki vifaa vitakavyo wasaidia kutumia Nishati Safi ya Kupikia.
Kupitia
sherehe hizo za tuzo za Malkia wa Nguvu 2025 wanawake mbalimbali wametambuliwa
mchango na harakati zao katika jamii na kupatiwa tuzo.
Na. Ofisi ya
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati




0 Maoni