Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), likiongozwa na Kamishna wa Uhifadhi Musa Nassoro Kuji, limeshiriki hafla ya Maadhimisho ya Kumbukizi ya Miaka 103 ya kuzaliwa kwa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius K. Nyerere, leo Aprili 13, 2025, yanayofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Dkt. Jakaya Kikwete, jijini Dodoma.
Hafla hiyo imehudhuriwa na
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Isdori
Mpango, pamoja na viongozi mbalimbali wa Wizara ya Maliasili na Utalii
wakiongozwa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Danstan Kitandula
(Mb).
Sherehe hizo zimeandaliwa na
Taasisi ya Kumbukumbu ya Mwl. J.K. Nyerere, ambapo TANAPA ni Mdhamini Mkuu wa
Maadhimisho hayo. Kaulimbiu ya Maadhimisho haya ni: “Chagua Viongozi Bora kwa
Ustawi wa Jamii na Maendeleo Endelevu ya Taifa.”
Katika kuenzi misingi ya
uongozi wa Mwalimu Nyerere na Azimio la Arusha ambalo lililenga kujenga jamii
yenye misingi ya uadilifu, usawa, uwajibikaji na uzalendo limekuwa likienziwa
hivyo kupitia maadhimisho hayo, Watanzania wamehimizwa kuendeleza maono ya Baba
wa Taifa kwa kusimamia rasilimali za nchi kwa manufaa ya kizazi cha sasa na
kijacho, sambamba na kuchagua viongozi bora watakaoendeleza misingi hiyo kwa
maendeleo endelevu ya Taifa.
Aidha, TANAPA imetumia
jukwaa hilo kuhamasisha Watanzania kupigia kura Hifadhi za Taifa kumi (10)
zilizoingia katika vipengele vinane (8) katika kuwania Tuzo kubwa za Utalii
Duniani, maarufu kama World Travel Awards, ili kuendelea kuitambulisha Tanzania
kimataifa jambo linalotarajiwa kuchochea ongezeko la watalii na mapato
yatokanayo na shughuli za utalii.
0 Maoni